TPA yapata tuzo ubora wa huduma

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:41 PM Sep 13 2024
TPA yapata tuzo ubora wa huduma
Picha: TPA
TPA yapata tuzo ubora wa huduma

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetunukiwa tuzo ya ushindi wa jumla katika Maonesho ya 19 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Furahisha, jijini Mwanza na kushirikisha zaidi ya taasisi 200 kutoka nchi wanachama.

Akizungumza wakati wa kutoa tuzo kwa TPA, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, alisema tuzo hiyo ya TPA imetokana na uboreshaji wa huduma katika bandari inazozisimamia kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika. 

Waziri Jafo alisema TPA imekuwa mshindi wa kwanza kati ya  Taasisi za Serikali zilizoshiriki kwenye maonesho hayo kwa kuwa na banda bora lenye kuvutia zaidi katika maonesho hayo. 

“Mafanikio haya ni matokeo ya usimamizi mzuri unaofanywa na TPA ikiwamo uwekezaji unaofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam,” alisema. 

 Maonesho hayo yenye kaulimbiu  ya "Uboreshaji wa Mazingira ya Uwekezaji na Biashara ni Kichocheo Katika Kukuza Uchumi wa Nchi" yana lengo la kukuza fursa za biashara na kuziwezesha nchi wanachama wa Afrika Mashariki kuchangamkia fursa ya masoko ya jumuiya nyingine ikiwamo vile SADC. 

Akifungua maonesho hayo, Waziri Jafo alisema malengo ya serikali ni kuboresha upatikanaji wa huduma katika sekta mbalimbali zikiwamo miundombinu ya barabara, reli na anga ili kukuza ukuaji wa biashara na uchumi. 

Jafo alisema uwekezaji mkubwa umefanyika katika bandari za Dar es Salaam, Mwanza na maeneo mengine ili kurahisisha wafanyabiashara wa ndani na  nje ya nchi kusafirisha biashara zao kwa haraka na kuchochea ukuaji wa uchumi. 

Akitolea mfano Bandari ya Dar es Salaam, alisema uwekezaji uliofanyika katika bandari hiyo ambayo ni kiungo kikubwa kwa  nchi nane zisizo na pwani katika Afrika Mashariki, Kusini na Kati kumeongeza ufanisi mkubwa katika kuhudumia shehena za meli za mizigo zinazotia nanga bandarini hapo. 

Bandari ya Dar es Salaam pia ni kiungo muhimu cha usafirishaji wa mizigo kwenda Mashariki ya Kati, Ulaya na hata bara la  Amerika. 

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa mamlaka hiyo, Leonard Magomba, alisema mamlaka sasa ina malengo zaidi ya  kuboresha bandari zake zingine kupitia upanuzi wa miundombinu, uwekezaji katika vifaa, na kuajiri wataalamu ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya kimataifa vya utoaji huduma. 

“Kwa sababu ya uwekezaji huu mkubwa, Bandari ya Dar es Salaam sasa inaweza hata kupokea meli kubwa zenye urefu wa hadi mita 300. 

“Hii imewezekana kwa kupanua kina cha lango la kuingia bandarini na eneo la kugeuzia meli, hali inayowezesha meli kubwa kutia nanga kwa urahisi zaidi," alisema Magomba.