RC Macha: Rais Samia yupo 'serious' na kilimo

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 04:01 PM Sep 13 2024
news
Picha:Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye kikao cha RCC

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan yupo “serious” na masuala ya kilimo, na amekuwa akitoa kipaumbele kwenye mambo mengi, ikiwamo na kuwawezesha maofisa ugani vitendea kazi,na sasa yupo kwenye ujenzi wa nyumba kwa maofisa ugani ngazi ya kijiji ili wawe karibu na wakulima muda wote.

Macha amebainisha hayo leo Septemba 13,2024 wakati akifungua kikao cha kamati ya ushauri mkoa wa Shinyanga (RCC).

Amesema Rais Samia kwenye utawala wake amefanya mambo makubwa katika sekta mbalimbali, na kwamba kwenye masuala ya kilimo amekuwa “serious” na ametoa vitendea kazi kwa maofisa ugani, ili wawe karibu na wananchi na kuwafikia virahisi na kuwapatia elimu ya kilimo chenye tija.

“Rais Dk. Samia Suluhu Hassan yupo serious kwenye masuala ya kilimo na hapa Shinyanga ametoa vitendea kazi kwa maofisa ugani, zikiwamo pikipiki,vishikwambi 262 kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za wakulima na “pair” 234 sare za kilimo na vifaa vya kupimia udongo,”amesema Macha.

Amesema pia kuna mkakati wa maofisa ugani wa vijiji vyote kujengewa nyumba, na kwamba katika mkoa wa Shinyanga tayari nyumba 4 za mfano zipo kwenye hatua ya manunuzi kwa ajili ya kujengwa, lengo likiwa waishi huko huko kwa wakulima. 

Aidha, ametoa wito kwa wakulima kwamba katika msimu ujayo wa kilimo 2024/2025 wafaute ushauri wa wataalamu na kulima kilimo chenye tija, sababu maofisa ugani wapo na wawatumie na wanavitendea kazi vyote zikiwamo pikipiki na kuwafikia kirahisi.

Amesema katika msimu wa kilimo uliopita 2023/2024 mkoa huo haukufanya vizuri kwenye zao la pamba na tumbaku, na kwamba kwenye pamba malengo ilikuwa ni kuvuna kilo milioni 30, lakini zimevunwa milioni 20.8, na upande wa Tumbaku matarajio ilikuwa kuvuna kilo milioni 16.5 lakini zimekomea kilo milioni 10.3.

Amesema zipo sababu mbalimbali ambazo zimesababisha mavuno hayo kuwa chini, ikiwamo kukithiri kwa mvua nyingi pamoja na wakulima kulima kimazoea na kupata mavuno kidogo.

“Mkakati wa mkoa mwezi wa 10 ukifika kwenye maandalizi ya kilimo kwa msimu ujayo, elimu itaanza kutolewa kwa wakulima ili walime kilimo chenye tija, hata kama bei ya pamba ikiwa chini lakini mkulima akilima kilimo cha kisasa na kupata kilo 1,500 hadi 1,750 kwa hekali, kama alivyopata mkulima wa Igunga atauza pamba yake na kuinuka kiuchumi, kuliko kulima kimazoea na kukomea kilo 100,200 na 300,”amesema Macha.

Amegusia pia suala la kilimo cha zao la mpunga, kwamba wakulima wamepata mavuno mengi, lakini changamoto hakuna soko la uhakika, ambapo wakulima huliuza kwa soko huria ambalo wanapunjika, na kutoa wito kwao wasiuze kiholela bali wahifadhi na chakula. 

Katika hatua nyingine Macha, amesema ndani ya miezi mitatu Rais Samia katika mkoa huo ametoa sh.bilioni 101.2 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kiwango cha lami kilomita 75 kutoka Kahama-Kakola, na kwamba barabara hiyo itakapokamilika itafungua fursa nyingi za kiuchumi.

Amesema kwa upande wa ujenzi wa madaraja pekee ametoa Sh.bilioni 14.3 na yatafanyiwa ukarabati pia yale madaraja ambayo yaliathiriwa na mvua.

Pia, amesema katika sekta ya maji tayari kuna mkataba wa sh. bilioni 45 ameshasainiwa ili kupeleka maji Ushetu, na hatua ya kwanza zitanufaika kata 9.

Nao baadhi ya wajumbe wa kikao hicho, wamepongeza hatua ya maendeleo ambayo inaendelea kutekelezwa mkoani humo chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye amekua akitoa fedha nyingi na kutekelezwa miradi mbalimbali ya maendeleo.