Wauawa madai kuvamia kituo cha polisi

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 10:51 AM Sep 13 2024
Msemaji wa Jeshi hilo Makao Makuu Dodoma, Naibu Kamishna (DCP) David Miseme
Picha: Mtandao
Msemaji wa Jeshi hilo Makao Makuu Dodoma, Naibu Kamishna (DCP) David Miseme

JESHI la Polisi limesema limewaua watu wawili kwa risasi wakati wa vurugu zilizotokea katika Kituo cha Polisi Lulembela, Mbogwe mkoani Geita.

Vurugu hizo zinadaiwa kufanywa na zaidi ya wananchi 800 waliovamia kituo hicho wakiwataka watu waliohisi kuwa wezi wa watoto.

Waliouawa katika vurugu hizo wametajwa kuwa ni pamoja na mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Lulembela, Teresia John (18), mkazi wa eneo jirani na kituo hicho cha polisi na mwanamume anayekadiriwa kuwa na miaka 18 hadi 20 ambaye majina yake hayajatambulika.

Taarifa iliyotolewa juzi na Msemaji wa Jeshi hilo Makao Makuu Dodoma, Naibu Kamishna (DCP) David Miseme, ilibainisha chanzo cha vurugu hizo ni watu wawili walioonekana wakiwa wamebeba watoto wawili katika eneo la mnada wa Lulembela na kuhofiwa na wananchi hao.

“Vurugu hizo zilianza katika mnada kisha kuhamia katika kituo cha polisi majira ya saa 8:39 mchana ambako wananchi hao baada ya kuona watu waliobeba watoto, waliwahisi kuwa wezi wa watoto na kuanza kuwashambulia,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya kuanza kuwashambulia, alitokea Mtendaji Kata ambaye aliwabeba kwenye pikipiki na kuwakimbiza katika kituo cha polisi.

“Baada ya watu hao kufika katika kituo cha polisi watu wanaokadiriwa kuwa 800 walifika kituoni hapo na kuwataka askari polisi wawakabidhi ili wawaue,” iliongeza taarifa hiyo.

Baada ya hapo inadaiwa kuwa, polisi waliwazuia na kuwaelimisha juu ya makosa ya kujichukulia sheria mkononi lakini wananchi hao walianza kushambulia kituo cha polisi kwa mawe wakitaka watolewe.

“Mbali na kushambulia kituo na kutaka kuingia ndani, wananchi hao walichoma moto gari moja lenye usajili namba T.440 ATW aina ya Toyota Cardina lililokuwa  limeegeshwa nje ya kituo hicho,” ilibainisha taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema baada ya kuwapo kwa hali hiyo,  askari walianza kutumia mabomu ya machozi na baadaye silaha za moto kwa kupiga risasi juu ili watu hao watawanyike hali iliyosababisha kuuawa kwa watu wawili waliokuwa katika eneo hilo.

Hata hivyo, ilibainika kuwa watu hao walikuwa wamebeba watoto wao na wala hakuna aliyekuwa ameiba mtoto. Taarifa  ilibainisha kuwa Emanuel John (33) alikuwa amebeba mtoto wake Ikram Emanuel (mwaka mmoja na miezi 11) na  Ng’amba Leonard (24) alikuwa amembeba John Emanuel mwenye umri wa miaka miwili na miezi minane. 

Mama wa watoto hao, Rachel Masunga (22) alithibitisha kuwa watoto hao ni wake na walikuwa kwa wifi yake walipofuatwa na baba yao mzazi na mjomba wao.

DCP Misime katika taarifa hiyo alisema jeshi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo sambamba na kukamata wanaodaiwa kuhusika katika vurugu zilizosababisha vifo hivyo.