Watoto 30 wafanyiwa upasuaji wa moyo

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 03:31 PM Sep 13 2024
Miongoni mwa wataalamu kutoka Saudi Arabia, waliohusika katika kambi ya siku 10.
Picha:JKCI
Miongoni mwa wataalamu kutoka Saudi Arabia, waliohusika katika kambi ya siku 10.

KITUO cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saudi Arabia kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kwa pamoja wamekamilisha kambi ya upasuaji moyo kwa watoto 30, akiwamo mtoto mchanga wa siku tatu.

Katika awamu tano za kambi za msaada za matibabu aina hiyo nchini, zilizofanywa na kituo hicho zimegharmu takribani Sh. bilioni nne.

Aidha, kambi ya awamu hii iliyokamilishwa jana, watoto 50 walifanyiwa uchunguzi na kati yao 30 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo ikigharimu Sh. milioni 700. .

Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI katika kufunga kambi ya siku 10, Dk. Tatizo Waane, alisema jijini Dar es Salaam kwamba huduma hiyo imetolewa chini ya Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu cha nchini Saudi Arabia.

“Matibabu haya ni muhimu kwa ajili ya afya kwa watoto na kuokoa gharama kwa pamoja wataalamu kutoka kwa Mfalme Salman na wa kwetu JKCI wameshirikiana. Kwa awamu hii wamedtoa matibabu ambayo gharama yake ni Sh. milioni 700. Jumla tangu waanze huduma hii imegharimu takribani Sh bilioni nne,” alisema Dk. Waane.

Balozi wa Saudi Arabia nchini, Bin Ahmed Okeish, alisema ni mpango wa kujitolea uliofadhiliwa na Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu, ambao ni mradi pia unaotekelezwa na cnhi zingine duniani.

 “Hadi sasa Saudi Arabia imetoa msaada unaofikia dola bilioni 108 katika nchi 169 duniani, na miradi ya kiutu iliyotekelezwa ni 6,898. Kwa Tanzania watoto wapatao 300 wamenufaika ” Bin Ahmed alisema

Balozi wa Saudi Arabia nchini, Yahaya Ahmed Okeshi (mwenye kanzu), akiwa pamoja na wataalamu wa afya wa JKCI na wenzao kutoka Kituo cha Misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman cha nchini Saudi Arabia, baada ya kufunga kambi maalumu ya matibabu ya siku 10 iliyokuwa ikifanywa na wataalamu hao katika taasisi hiyo. PICHA: JKCI
Mkurugenzi kutoka Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdullah Kilima, alisema huduma hiyo ni miongoni ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika huduma za tiba kidiplomasia.

Awali, Mkurugenzi wa Upasuaji na Biingwa wa Usingizi na Wagonjwa Mahututi kutoka JKCI, Dk. Angela Muhozya, alisema kambi hiyo ni mwendelezo wa ushirikiano mzuri kati ya nchi hizo mbili, na kwamba mtoto huyo mchanga wa siku tatu, mishipa yake ya moyo haikuwa katika mpangilio sahihi.

“Tunawashukuru wenzetu wa Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kwa kujitoa kwao, kwani licha ya kutoa huduma za matibabu pia wametupatia vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500 ambavyo vinatumika katika kufanya upasuaji huu wa moyo,” alisema Dk. Angela.

1
Bingwa wa Moyo na Mishipa ya Damu kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu, Dk. Mohammad Shihata, alisema kambi hiyo imekuwa ikidhaminiwa na Mfalme Salman wa nchini Saudi Arabia, kuwawezesha watoto kupata matibabu na kubadilishana ujuzi na madaktari wa JKCI.

Alisema timu nzima ya watu 26 kutoka nchini Saudi Arabia ambao ni waatalamu wa usingizi, waendesha mashine za moyo, wauguzi na madaktari wameshiriki katika kambi hiyo, ili kuhakikisha watoto wengi wanafanyiwa upasuaji wa moyo.

“Hii ni siku yetu ya tano na ni mara ya yangu ya saba kuja hapa nchini kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto, siku zote tumekuwa tukipokea ushirikiano mzuri kutoka kwa madaktari wa JKCI katika kufanikisha utoaji wa huduma hii,” alisema Dk. Shihata.