Wamlilia waziri gharama kubwa za matibabu MOI

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 11:10 AM Sep 13 2024
Waziri wa Afya, Jenister Mhagama (katikati), akimsikiliza mkazi wa Songea mkoani Ruvuma, Jafari Malingizi, alipotembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Ubongo Muhimbili (Moi) leo Septemba 11, 2024.
Picha: Mtandao
Waziri wa Afya, Jenister Mhagama (katikati), akimsikiliza mkazi wa Songea mkoani Ruvuma, Jafari Malingizi, alipotembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Ubongo Muhimbili (Moi) leo Septemba 11, 2024.

BAADHI ya wagonjwa wanaopatiwa huduma katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), wamemweleza Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, changamoto wanazokumbana nazo hasa gharama kubwa za matibabu.

Wagonjwa hao, ndugu na jamaa zao, walisema hayo kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam, baada ya Waziri Mhagama kufanya ziara MOI na kuwataka kutoa madukuduku yao kuhusu huduma hospitalini hapo.

Mmoja wa wananchi hao, Abdallah Shaaban, alisema ili kufanikisha matibabu ya ndugu yake, imempasa kuuza baadhi ya mali kwa ajili ya kulipia gharama za matibabu.

“Mama yangu kalazwa hadi sasa huduma ni Sh. milioni mbili. Nimetoa Sh. 600,000 nimeuza mahindi, mimi ni mkulima. Naomba  serikali inione mtu kama mimi napata wapi hela hadi sasa nimeshatoa zaidi ya Sh. milioni mbili,” alisema.

Thadei Kivamba alisema anaiomba serikali iwapunguzie wananchi gharama za huduma tofauti, kama vile ya kulaza mgonjwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU), inayofikia Sh. 80,000 kwa siku.

“Nimetoka Tosamaganga mkoani Iringa,  mgonjwa wangu kitanda kulala ICU ni Sh. 80,000 kwa siku. Kwa  Mtanzania wa kawaida, anapata wapi fedha hii? Hapo  bado vipimo, dawa na kumwona daktari bingwa,” alisema Kivamba.

Amina Baraka, alisema mgonjwa wake kafanyiwa upasuaji wa kichwa gharama hadi sasa imefikia Sh. milioni sita, ikimuwia vigumu kulipa.

“Mgonjwa wangu kafanyiwa upasuaji wa kichwa. Tuliuza  vitu nikaja na Sh. milioni tatu na deni ni Sh. milioni nne, bado dawa nimeambiwa Sh. 100,000 jana (juzi),” alilalamika. 

Akijibu hoja hizo, Waziri Mhagama alisema lengo la serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora, kwa kuchangia gharama kidogo ikilinganishwa na hospitali binafsi.

“Tunasisitiza ni mgonjwa akifika apewe huduma kwanza, mengine yanakuja baadaye. Okoa maisha kwanza ya mgonjwa halafu deni lifuate, tunatarajia kukamilisha kanuni za Bima ya Afya Kwa Wote, ambayo itasaidia kupunguza gharama za matibabu,” alisema Mhagama. 

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Lemeri Mchome, alisema gharama za huduma haziepukiki kwa kuwa fedha zinahitajika kwa ajili ya uendeshaji na kufanyia ukarabati mashine za vipimo vya kisasa.

“Huduma ya afya haitolewi bure kwa sababu kila mmoja anatakiwa kuchangia ili kufanya iwe endelevu. Mfano kufanya upasuaji wa kichwa MOI kwa mgonjwa mmoja ni takribani Sh. 600,000 baadhi ya hospitali binafsi inafikia hata Sh. milioni 20,” alisema Dk. Mchome.