MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, amesema uzinduzi wa huduma ya upandikizaji mimba (IVF) ni msaada mkubwa kwa wananchi na familia zilizokumbana na changamoto ya uzazi kwa muda mrefu.
Alisema awali ilipatikana nje ya nchi kwa gharama kubwa na sasa huduma ya IVF nchini inatarajiwa kugharimu takribani Dola za Marekani 5,000 (sawa Sh. 13,611,700) kulingana na aina ya matibabu.
Alisema hayo jijini Dar es Salaam, wakati akizindua jengo la Upandikizaji Mimba (IVF), kupokea gari la kliniki tembezi (mobile clinic van) pamoja na kuwasha mashine za vifaa vya usikivu kwa watoto 14 (cochlear implant) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
“Ni wakati wa nchi kujitegemea katika tiba za kibobezi zinazotolewa na wataalamu wa ndani ili kuwapunguzia gharama kubwa za matibabu ya kibingwa Watanzania.
“Serikali itaendelea kujivunia na kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani namna ya kuvitumia vifaa vya matibabu ya kibingwa pamoja na kupatiwa ujuzi wa kuvikarabati pindi itakapohitajika,” alisema Dk. Mpango.
“Mradi huu ulianza mwaka 2019 na umegharimu Sh. bilioni 1.1 mapato ya ndani. Ni faraja kubwa huduma ya upandikizaji IVF kuanza kutolewa kwa mara ya kwanza nchini katika hospitali za umma, awali ilipatikana hospitali binafsi pekee, Arusha na Dar es Salaam, wengine wakienda Afrika Kusini, Uturuki au Kenya.”
Kuhusu huduma ya upandikizaji vifaa vya usikivu, kabla ya mwaka 2017, alisema awali haikupatikana nchini na iliwalazimu wenye mahitaji kwenda nje ya nchi kwa matibabu, hatua ya kuanza kwa huduma hiyo ni kuwapunguzia gharama wananchi za kufuata matibabu ya kibobezi nje ya nchi.
“Nawaomba wataalamu wetu wazingatie watoto hawa kujifunza kuzungumza ‘speech therapy’ ili watoto waliopandikizwa ‘cochlear implant’ waanze kuzungumza,” alisema Dk. Mpango.
Alisema hatua ya MNH kuwa na gari la kliniki tembezi, itaboresha huduma na kuwafikia wagonjwa walipo, pamoja na kukamilisha azma ya hospitali za matibabu ya kibingwa kufanya huduma za aina hiyo mara nne kwa mwaka.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi, alisema mradi wa IVF utaanza kwa kuwapandikiza mimba kinamama 10 ambao wamekwishaanza kliniki, kuna wataalamu 10 na uwezo wa kituo hicho ni kutunza mayai kwa zaidi ya miaka 30.
“Kama lilivyo jina letu la Hospitali ya Taifa tuliona familia kushindwa kupata mtoto au watoto kwa asilimia 35 yanatoka upande wa wanaume na asilimia 65 ni wanawake, kutokana na tafiti mbalimbali,” alisema Prof. Janabi.
“Kwa hospitali yetu MNH kila siku katika wagonjwa 10 tunaowaona kliniki ya kinamama watatu hadi wanne wana tatizo la uzazi. Asilimia 30 ya wagonjwa tunaowaona wana tatizo. Baada ya kuona kuna masononeko katika nyumba zetu, tulifanya maamuzi kununua vifaa vilivyogharimu Sh. bilioni 1.1.”
Alisema kwa wanawake ambao kwa sasa hawako tayari kupata watoto aidha kuwa masomoni, wanaweza kuhifadhi mayai yao kituoni hapo na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo na kwamba MNH itaendelea kuwaalika wataalamu mbalimbali kutoka nje.
Kuhusu mradi wa gari ya kliniki tembezi ambalo MNH wameipata, alisema usafiri umegharimu dola 200,000 na kwamba hatua hiyo itatimiza utoaji huduma za kuwafikia wananchi pale walipo.
Katika mradi wa upandikizaji vifaa vya usikivu watoto 14, Prof. Janabi alisema idadi hiyo inafikisha waliopandikizwa kufikia 84 na 73 kati yao wakipandikizwa masikio yote mawili na 11 wamepandikizwa sikio la upande mmoja.
“Watoto hawa 14 leo (jana) wanapata fursa ya kusikia kwa mara ya kwanza, katika jamii watoto wa aina hii huadhibiwa kwamba ni watukutu kumbe tatizo ni usikivu. Tumeanza na hawa 14 kwa gharama ya Sh. milioni 345 na wengine 24 watafuata kupata huduma hii,” alisema.
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, alisema lengo la serikali ni kuhakikisha huduma ya Afya Kwa Wote inawafikia wananchi wote, ili kuwapunguzia gharama za matibabu ikiwamo ya kibingwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED