ERB yagharamia walimu 20 kufundisha sayansi shule tatu

By Joyce Lameck , Nipashe
Published at 05:22 AM Aug 27 2024
Msajili wa Bodi ya Wahandisi Tanzania, Mhandisi Bernard Kavishe.
Picha: Mtandao
Msajili wa Bodi ya Wahandisi Tanzania, Mhandisi Bernard Kavishe.

BODI ya usajili wa Wahandisi (ERB), imepeleka walimu 20 wa masomo ya fizikia na hisabati katika shule tatu, ili kusaidia serikali kuongeza idadi ya walimu wa masomo hayo na kuongeza mwamko wa wanafunzi kuyapenda.

Aidha, ERB imeomba wadau kuwaunga mkono katika mbio za marathoni zitakazofanyika Dar es Salaam Septemba 6,mwaka huu, kwa ajili ya kupata fedha za kulipa posho walimu wa kujitolea wa masomo ya sayansi katika shule mbalimbali nchini,ambazo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.

Akizungumza na waandishi wa habari, jana Mkoani Dar es Salaam, Msajili wa Bodi ya Wahandisi Tanzania, Mhandisi Bernard Kavishe, alisema lengo ni kupeleka takribani walimu 100 wa kujitolea katika shule 26 nchini,ambao watagharamiwa na ERB.

"Hadi sasa walimu 20 wako ubaoni (wanafundisha) katika shule tatu katika mikoa ya Kagera,Geita na Dar es Salaam.ERB inawagharamia posho,nauli na bima ya afya,"alifafanua.

Aidha,aliwaomba wadau nchini kushiriki katika mbio hizo, kuwa zipo njia nne ambazo zitatumika ili kufanikisha mradi huo utakao wasaidia walimu, ambao watatarajiwa kuwaajiri katika shule mbalimbali.

Mhandisi Kavishe alisema Septemba 3 na 4 mwaka huu, kutakuwa na kongamano la vijana katika tasinia hiyo, wakieleza umma ni kwa namna gani wanafanya kazi zao.

Vile vile Septemba 5, litafanyika kongamano litakalo jumisha takribani watu 6,000, kati ya hao wahandisi watakuwa 4,000 na wengine 2,000 si wahandisi.

Aidha, Septemba 6,mwaka huu, itakuwa ni siku ya kilele ambapo kutakuwa na mbio za marathoni zitakazohusisha wahandisi kutoka nchi nzima.

“Zipo njia nne za kushiriki ya kwanza kimbia upate afya, njia ya pili kama huna mbio unaweza kukadhamini wakimbiaji, njia ya tatu unaweza ukalipia jezi hizi tunadaiwa, pia njia ya nne ni kununua vifurushi vya walimu wale,” alisema hayo Mhandisi Kavishe.

"Walimu wale tunawalipia posho ya kila mwezi, tunawalipia bima ya afya na tunawapa nauli ya kwenda kituo cha kazi, pia wakati wa likizo anapokwenda kwao na mwalimu mmoja anaweza tugharimu laki tisa,"alifafanua.

Alisema ERB imeamua kushiriki mchakato wa kuwaandaa wahandishi kuanzia ngazi za awali za elimu kwa kuwafanya wanafunzi wapende masomo ya sayansi,kwa kupeleka walimu ambao wataamsha ari ya kusoma masomo hayo.

"Tulifanya utafiti na kubaini kuwa tunapaswa kuandaa wataalam tangu ngazi za chini kabisa,tulibaini kuna upingufu wa walimu wa fizikia na hisabati.Tumekuja na mpango wa kutafuta fedha za kugharamia walimu wa kujitolea,tunaunga mkono jitihada za serikali kuhakikisha walimu wanakuwepo wa kutosha.

"Tunaomba wadau wajitokeze kutuunga mkono ili kupitia mbio hizo tupate fedha za kugharamia walimu zaidi watakaokwenda kufundisha masomo hayo kwenye shule ambazo tumeshazitambua,"alisema.

Kwa mujibu wa Kavishe,serikali imejenga miundombinu ya elimu katika ngazi mbalimbali,imetoa nafasi kwa wadau kugharamia walimu wa kujitolea,nasi tupo tayari kuhakikisha tunachangia uandaaji wa wahandisi tangu ngazi za awali.

Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Wahandisi Kitengo cha Wanawake, Mhandisi Ester Christopher, alisema wamekuwa wakihamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya fizikia, kutokana na kwamba kuna uwiano mdogo kati ya wanaume na wanawake katika tasnia ya uhandisi nchini.

Vile vile, alisema baada ya kutembelea shule mbalimbali waligundua kuwa wanafunzi wakike hawana taarifa sahihi, ambazo zitawahamasisha kupenda masomo ya fizikia na hisabati ili baadaye kuwa wahandisi.

“Tulichogundua ni kwamba wanakosa mwongozo au ile picha ya kuona kuwa kuna wahandisi wanawake, hivyo tukaona tuwafuate hao mabinti kuwa suluhisho ni lazima wapende masomo ya fizikia na waje wengi kwenye tasinia ya uhandisi, ili tupate suluhisho ambalo linamgusa moja kwa moja,"alisema mhandisi Ester.

Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwerwa, mkoani Kagera, Mwalimu Ndabazi Stephano, alisema kuwa wahandisi ni lazima waandaliwe tangu wakiwa ngazi za chini kabisa za elimu, ili kupata wanataaluma mwenye uweledi katika tasnia hiyo.

Aidha, alisema kuwa baada ya ERB kupeleka walimu wa masomo ya fizikia na hisabati, kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wanafunzi kusoma masomo hayo na kuwa watoto wa kike wameamka kwa wingi zaidi tofauti na awali.