Marekani yasisitiza nia ya kushiriki kuendeleza Mradi wa Kabanga Nickel, BHP

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:20 PM Aug 27 2024
Serikali ya Marekani imesisitiza nia ya kushiriki katika kuendeleza Mradi wa Kabanga Nickel na Kampuni ya BHP.
Picha:Mpigapicha Wetu
Serikali ya Marekani imesisitiza nia ya kushiriki katika kuendeleza Mradi wa Kabanga Nickel na Kampuni ya BHP.

Serikali ya Marekani imesisitiza nia ya kushiriki katika kuendeleza Mradi wa Kabanga Nickel na Kampuni ya BHP.

Pia  imeweka  mkazo wa ushiriki wake katika mradi huo wa kimkakati ambao ni kati ya miradi mikubwa na kielelezo katika sekta ya madini nchini.

Hayo yamesemwa na  Waziri wa Madini Anthony Mavunde ambae amefanya mazungumzo na kampuni ya Tembo Nickel ambayo Serikali ya Tanzania ni Mbia ili kupokea ujumbe maalum kutoka kwa Kampuni mama ya Tembo Nickel pamoja na Serikali ya Marekani kupitia kwa Balozi wa Marekani nchini Tanzania Balozi Battle na ujumbe wa Marekani uliobebwa na Helaina Matza, Mratibu Maalum wa Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa Ajili ya Mpango maalum wa Nchi saba zilizoendelea zaidi Kiuchumi duniani G7.

Katika ujumbe huo uliowasilishwa  Matza umebeba malengo ya  kuwezesha miradi mbalimbali ya kimkakati (PGII) na pia unathibitisha kuwa nchi ya Tanzania ni nchi inayovutia wawekezaji na mazingira ya uwekezaji ni rafiki na hii imechochewa sana falasafa ya uongozi wa  Rais Samia Hassan ya 4R-Reconciliation(Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reform (Mabadiliko) na Rebuilding  (Kujenga upya).

Akizungumza katika mkutano huo Waziri Mavunde ametoa shukrani kwa Rais Samia  kwa kuimarisha zaidi uhusiano na Marekani ambao ndio umeleta mafanikio haya. 

"Mafanikio haya yanatokana na mikakati ya Mh. Rais katika mashauriano yake kwenye Mkutano wa Marekani na Afrika uliofanyika mwaka 2022 na pia ujio wa Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris wakati wa ziara yake Tanzania mwezi Machi 2023," amesema.

Aidha,  Mavunde alipata wasaa wa kukutana na Afisa Mkuu wa Maendelezo wa Kampuni ya BHP , Catherine Raw aliyekuja nchini kutizama maendeleo ya Mradi wa Kabanga Nickel na kuisisitizia Serikali ya Tanzania nia ya kushiriki katika kuendelea Mradi huu ambao unaenda sambamba na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kusafisha madini kitakachojengwa Wilayani Kahama,Mkoa wa Shinyanga uwekezaji utakaogharimu zaidi ya Dola Milioni 500.