MNH-Mloganzila yawapandikiza 30 nyonga, magoti

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 10:22 AM Aug 27 2024
MNH-Mloganzila yawapandikiza 30 
nyonga, magoti
Picha:Mpigapicha Wetu
MNH-Mloganzila yawapandikiza 30 nyonga, magoti

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, imeanza kuwafanyia upasuaji wa kupandikiza nyonga na magoti wagonjwa 30, kuanzia Agosti 26 hadi 30, mwaka huu.

Upasuaji huo, unafanywa na wazawa mabingwa na bobezi wa upasuaji nyonga na magoti kutoka MNH-Mloganzila, wakishirikiana na Bingwa Bobezi kutoka India, Dk. Venuthuria Ram Mohan Reddy.


Akizungumza kuhusu kambi ya upasuaji na upandikizaji huo, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Mohamed Janabi, alisema huduma hiyo ilianza hospitalini hapo tangu mwaka 2022 na tayari 173 wamefanyiwa upandikizaji.


“Wagonjwa 173 wameshafanyiwa upasuaji, wataalamu tunao sita na huwa tunashirikiana na wenzetu kutoka nje. Serikali inalenga kujenga uwezo wa ndani, ili kuwapo na sehemu zaidi za huduma hii nchini.


“Kuna ongezeko la tatizo hili hasa kwa vijana. Nchini wamefanyiwa wengi, akiwamo Sunday Manara aliyewahi kucheza timu ya Yanga na nyingine. Sasa anaona matokeo ya upasuaji huo.


“Duniani upasuaji huu si kitu kigeni na kipya, wamefanyiwa upasuaji watu maarufu na wanaendelea na maisha yao kama kawaida. Mcheza filamu Arnold Schwarzenegger, mwanamuziki Lionel Richie, wamefanyiwa upasuaji wa magoti yote,” alisema Prof. Janabi.


Alibainisha kwamba kukua kwa teknolojia duniani, utaalamu ndio uhakika wa tiba hiyo unavyoongezeka na waliofanyiwa upasuaji hukaa kwa takribani miaka 20 akiwa vizuri.


“Kuumwa miguu na hadi upasuaji ni sawa, lakini kuteseka na ugonjwa si sawa, kwa sababu matibabu yapo. Kwa sababu kuendelea kutumia dawa za maumivu ni kuathiri viungo vingine,” aliongeza.


Kuhusu gharama, Prof. Janabi alisema ni kati ya Sh. milioni saba hadi 10 kutegemeana na ugonjwa na kwamba MNH itaendelea kuufanya na kujifunza kutoka kwa wengine waliofanya upasuaji zaidi.


“Gharama ni Sh. mil saba hadi 10 na wenye bima asilimia 90 ya huduma inalipiwa ndio maana tunahimiza bima kwa wananchi wakate, kabla ya ugonjwa, mtu, umri wowote mtu anaweza akaugua.


“Zamani wakati nasoma ilikuwa nikisia wenye ugonjwa huu, umri wao ulikuwa kama wa Mzee wangu (baba), lakini sasa umri wa miaka 30 au 40 ana tatizo la magoti, nyonga kwa sababu ya mtindo wa maisha. 


Ukiwa na kilo 120 zinazobebwa na magoti mawili itakuwa ni kwa muda tu na kitakachotokea ni kwenye viungio ‘joint’ kusagika,” alifafanua Prof. Janabi.


Bingwa Mbobezi wa Upasuaji wa Nyonga na Magoti kutoka Hospitali hiyo, DK. Abubakar Hamis, alisema kambi hiyo imeanza na huduma kwa wagonjwa sita kati ya 30 watakaohudumiwa kwa siku tano.


“Tatizo husababishwa na sababu mbili; kwanza ni umri mkubwa na uzito mkubwa. Wanawake wengi, hasa waliofika umri wa ukomo wa hedhi, ndio hupata tatizo zaidi.


“Wagonjwa wengi tuliokwisha wafanyiwa ni uzito na umri mkubwa.

Kwanza tunawapa dawa za maumivu na mwisho wa siku dawa hazifanyi kazi tena na nyonga kuweza kupinda au magoti, inabidi kufanyika upasuaji.


“Mwaka huu tunashirikiana na mtaalamu kutoka india na mara ya mwisho tulikuwa na wataalamu kutoka Uingereza,” alisema Dk. Abubakar.


Miongoni mwa walikwishapatiwa huduma hiyo, Manara (72), alisema Watanzania wanapopata tatizo la nyonga na magoti wasisite kutibiwa nchini na katika hospitali hiyo, kwa kuwa kuna wataalamu.


“Nina miaka 72 na ninajitahidi kuzingatia masharti na uzito usizidi na nisijitoneshe. MNH ina huduma nzuri. Wanamichezo wanaopata tatizo ni vyema kuja kuonana na madaktari kuliko kukata tamaa,” alisema Manara.