Prof. Janabi: Jamii ijihadhari na visababishi ugonjwa kiharusi, unene umo

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 06:19 PM Aug 27 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Janabi akizungumza na waandishi wa habari.
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Janabi akizungumza na waandishi wa habari.

PROFESA Mohamed Janabi, anasema ukubwa wa tatizo la kiharusi duniani unaongezeka, hasa kwa nchi zinazoendelea huku zaidi ya watu milioni 100 duniani kote wanaishi na ugonjwa huo, akitahadharisha jamii kuepuka visababishi.

Prof. Janabi ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba cha South Carolina cha nchini Marekani, anatoa elimu kupitia kitabu chake: Mtindo wa Maisha na Afya Yako, kuhusu uzito mkubwa na athari zake.

“Katika kipindi cha miaka 30 iliyopita matukio ya kiharusi yameongezeka maradufu. Mwaka 1990 wagonjwa wa kiharusi duniani kote walikuwa milioni 54 tu, lakini ilipofika mwaka 2019 idadi ya wagonjwa wa kiharusi ilipanda mpaka zaidi mpaka watu milioni 100.

Kinacholeta hofu kubwa kwetu ni kwamba asilimia 89 ya wagonjwa wa kiharusi, wako kwenye nchi zinazoendelea na zile za kipato cha kati. Kati ya hawa zaidi ya watu milioni 15 wanatoka katika bara la Afrika,” anaeleza bingwa huyo mbobezi katika magonjwa ya moyo.

Anasema taarifa za utafiti zinaonesha kwamba, hali inazidi kuwa mbaya kadri siku zinavyosonga huku kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2016, takwimu zikionesha kuwa mtu mmoja kati ya wanne ana tatizo la kiharusi. 

Pia, anasema hali hiyo ni tofauti na zamani kwa kuwa waliokuwa wanapata kiharusi walikuwa ni wazee wenye umri wa miaka 70 kuendelea na miaka ya hivi karibuni, asilimia 63 ya watu wanaopata kiharusi wana umri chini ya miaka 60.

“Tafiti za kitaalamu zimethibitisha kwamba, vipo visababishi vikubwa vitano vinavyochochea mtu kupata kiharusi. Hali hii ina athari sawa kwa wanaume na wanawake. Ingawa, mataifa mbalimnbali kulingana na viwango ya urefu wa maisha (life expectancy), wanaweza kutofautiana, visababishi hivi bado madhara ni sawa kwa watu wote.”

Anaeleza inaonesha kwamba kuna visababishi na kati ya watu kwa umri wa miaka 18 hadi miaka 54 kwa  wanaume na wanawake, hasa katika shinikizo la juu la damu (High Blood Pressure).

“Shinikizo la juu la damu, linaloongoza kwa umri wa makundi yote kuanzia miaka 18 hadi 34, miaka 34 hadi 44 na miaka 45 hadi 54. Hali hii ni ya kufanana kwa wanaume na wanawake.

Mafuta kuzidi mwilini, inatajwa kuwa kisababishi namba mbili kwa zote katika kusababisha watu kupata kiharusi. Tatizo hili makundi ya rika zote na huathirika. Kisukari, ni kisababishi namba tatu kinachosababisha mtu kupata kiharusi.”

Pia, anasema watu wanaovuta sigara kwa wingi wamo hatarini unavyochangia matatizo ya kiharusi kwa makundi ya rika zote na jinsi zote huku watu wenye uzito uliopitiliza

“Visababishi vikuu vilivyothibitika kuchangia viharusi ni pamoja na uzito. Kuweka puto (intragastric Balloon) ni teknolojia mpya ya uhakika ya kusaidia wagonjwa kupunguza uzito. 

Teknolojia hii ilipata idhini ya Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (Federal Food and Drags Authority -FDA) mwaka 2015. Mamlaka hii ndiyo inayoidhinisha matumizi ya mifumo mipya ya matibabu duniani. 

Utaratibu wa kuweka puto tumboni hautumii upasuaji, haingizwa kupitia mdomoni hadi tumboni. Wanaofaa kufanyiwa utaratibu ni wale wagonjwa wenye uzito uliopitiliza, yaani wenye uzito kuanzia kilo 90 kwenda juu au wale ambao kwa kipimo cha BMI cha zaidi ya 31.”