Manara aita wenye tatizo kama lake kufika MNH-Mloganzila

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 05:50 PM Aug 27 2024
Sunday Manara (72).
Picha:Mpigapicha Wetu
Sunday Manara (72).

MCHEZAJI wa zamani wa timu ya taifa ya mpira wa miguu nchini, Sunday Manara (72), amesema wachezaji wenzake wenye tatizo la nyonga na magoti, wasisite kufika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, kupata matibabu.

Manara, ambaye ni miongoni mwa wagonjwa 173  waliopatiwa matibabu aina hiyo hospitalini hapo, aliyasema hayo mkoani Dar es Salaam, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi ya upasuaji na upandikizaji wa nyonga na magoti.

Hospitali hiyo ilianza rasmi matibabu ya upasujai na upandikizaji wa nyonga na magoti, mwaka 2022 na imeshawafanyia huduma hiyo wagonjwa 173.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Mohamed Janabi, alisema kuna ongezeko la tatizo hilo hasa kwa vijana.

“Nchini wamefanyiwa wengi, akiwamo Manara aliyewahi kucheza timu ya Yanga na nyingine. Sasa anaona matokeo ya upasuaji huo.

“Duniani upasuaji huu si kitu kigeni na kipya, wamefanyiwa aupasuaji watu maarufu na wanaendelea na maisha yao kama kawaida. Mcheza filamu Arnold Schwarzenegger, mwanamuziki Lionel Richie, wamefanyiwa upasuaji wa magoti yote,” alisema Prof. Janabi.