Makalla ataja siri ushindi CCM Uchaguzi Serikali za Mitaa

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 04:28 PM Aug 27 2024
KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Amos Makalla.
Picha: CCM
KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Amos Makalla.

KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Amos Makalla amesema chama hicho kinategemea viongozi wa mashina, matawi na mabalozi katika kushinda Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.

Alisema hayo jana wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam, wakati akizundua Shina la Wakereketwa Wavuvi Beach Mjimwema, ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku tatu aliyoianza wilayani humo.
Agosti 19 mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa, alitangaza tarehe rasmi ya uchaguzi huo, akisema utashirikisha vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu.

Akizungumza na wanachama wa CCM jana wakati akindua shina hilo, Makalla alisema kuelekea uchaguzi huo CCM nguvu yake kubwa ipo katika viongozi hao ili kuibuka na ushindi.

Hivyo, aliwataka viongozi hao nchini kuhakikisha katika uchaguzi huo CCM kinaibuka na ushindi mkubwa na wa kishindo.

Makalla alisema: "CCM nguvu yake kubwa ipo katika viongozi wa mashina, matawi  na mabalozi. Hivyo kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tunawategemea sana viongozi hao. Pia CCM inategemea jumuiya zake ikiwemo Umoja wa Wanawake ( UWT) pamoja na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi ( UVCCM) kupata wanachama".

Kadhalika alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri itakapoanza kutolewa asiwasahau vijana wa CCM wa shina hilo.

Makalla alisema: "Vijana wajasiriamali wengine mnapaswa kuiga mfano wa shina hili walichokifanya. Pia tunatarajia ushindi mkubwa wa Serikali za Mitaa hapa Mjimwema kupitia shina hili".

Pamoja na mambo mengine, Makalla aliwachangia Sh. milioni moja wanachama wa CCM shina hilo Ili iwasaidie katika shughuli za shina hilo.