Dk. Mpango ataka udhibiti ‘school bus’

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 07:51 AM Aug 27 2024
MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango.
Picha: Mpigapicha Wetu
MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango.

MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, ametoa maagizo saba kwa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, mojawapo ni kuongeza udhibiti kwa magari yanayobeba wanafunzi (School bus), kwamba mengi hayakidhi vigezo vya kutembea barabarani na madereva wake wengi hawana weledi.

Agizo lingine ni wafuatilie ukaguzi wa mara kwa mara kwa magari yote, kufanya ukaguzi mara nne kwa mwaka.

Alitoa maagizo hayo jana wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani na miaka 50 ya Baraza la Taifa la Usalama Barabarani yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma.

“Jeshi la Polisi linapaswa kuongeza udhibiti wa mabasi ambayo yamekuwa yakitumika kubeba watoto wa shule, kwani mengi hayana sifa ni mabovu na mengine yanabeba watoto zaidi ya uwezo wake, lakini pia madereva wake wengi hawana weledi,” alisema Dk. Mpango na kuongeza:

“Madereva hao wamekuwa wakisababisha ajali za ovyo kama ile iliyotokea Aprili 12, mwaka huu, kule Arusha ambapo wazazi walipoteza watoto wao saba kwa uzembe. Ninawataka Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa dereva anayepewa leseni lazima awe amekidhi vigezo vyote”.

Dk. Mpango alisema Jeshi la Polisi linapaswa kutoa elimu ya usalama barabarani mara kwa mara ikiwamo kutanuliwa kwa makundi yote.

Kadhalika, aliwataka wananchi kuwa sehemu ya kukemea uvunjifu wa matukio ya ajali barabarani na siyo kukaa kimya.

“Jeshi la Polisi tumieni Tehama katika kukabili matukio ya usalama barabarani pia mwongeze udhibiti kwenye mabasi ya shule ambayo yamekuwa yakitumika kubeba wanafunzi, lakini mengi hayana sifa ya kutembea barabarani,” alisema Dk. Mpango.

Agizo lingine alilitaka Jeshi la Polisi kuwapa ajira zaidi madereva wanawake kwa sababu takwimu zinaonyesha matukio mengi ya ajali yanasababishwa na madereva wanaume kuliko wanawake.

Kadhalika aliwata watumiaji wa barabara wote wazingatie usafi wa mazingira, kwamba lisiwe jukumu la kikundi cha watu.

Aidha, alisema madereva wote wanaovunja sheria wanapaswa kuchukuliwa hatua kali bila kujali kuwa ni dereva wa serikali au binafsi.

Pia, alilitaka Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kuendesha doria za kushtukiza za kufanya ukaguzi wa magari pamoja na weledi wa madereva na wasiokidhi vigezo kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Dk. Mpango alisema kwa hali ilivyo sasa kama hatua madhubuti za kudhibiti ajali hazitachukuliwa utafiti unaonyesha kuwa ajali ndiyo itakuwa chanzo kikuu cha vifo ifikapo mwaka 2030.

“Taifa letu linapoteza nguvu katika kipindi cha mwaka 2023 katika ajali 1,733 zilizotolea vifo vilikuwa ni 1,647 na majeruhi ni 2,716, hivyo kama hatutachukua hatua basi ajali ndiyo itakuwa chanzo kikuu cha vifo ifikapo 2023,” alisema.

Kadhalika alisema ajali za pikipiki hivi sasa nchini zinaongezeka ambapo kwa kipindi cha mwaka 2023 zilikuwa 435, kusababisha vifo 376 ukilinganisha na vifo 332 kwa mwaka 2022.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, alisema katika kukabiliana na matukio ya ajali nchini wizara imetekeleza miradi mbalimbali ambayo itasaidia kupunguza hali hiyo.

Alisema moja kati ya miradi hiyo ni pamoja na ule wa miji salama wa kufunga kamera za usalama kwenye miji ambao utekelezaji wake upo katika hatua za mwisho.

Alisema mradi huo utakwenda kutekelezwa kwenye majiji ya Dodoma, Arusha, Mwanza na Dar es Saalam.

“Ni matumaini yetu kuwa miradi hii ikikamilika tutakwenda kudhibiti ajali hasa katika maeneo yasiyo na askari kutokana na kamera zitakazokuwa zimefungwa katika maeneo hayo,” alisema Masauni.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, alisema moja ya sababu ya kuongezeka kwa ajali barabarani ni makosa ya kibinadamu.

“Baadhi ya madereva hawazingatii masuala ya sheria za usalama barabarani, hivyo kufanya makosa ya kibinadamu na kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la ajali nchini kutokana na hali hiyo baraza tumeandaa mkakati utakaoshirikisha wadau wote na baada ya miezi tutafanya tathmini kuona hali ikoje,” alisema Sillo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Cumillius Wambura, alisema katika kukabiliana na ajali nchini wametekeleza maagizo mbalimbali ya serikali ikiwamo kufunga mifumo ya kisasa kudhibiti ajali barabarani.