Msajili ndani ya mgogoro wa TLP, kuufumua sasa

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 07:04 AM Jul 17 2024
Makamu Mwenyekiti TLP, Dominatha Rwechungura akizungumza kuhusu mikakati ya chama.
PICHA: SABATO KASIKA
Makamu Mwenyekiti TLP, Dominatha Rwechungura akizungumza kuhusu mikakati ya chama.

MGOGORO wa kiuongozi ndani ya Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), huenda ukapata ufumbuzi baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa, kupanga kuushughulikia kuanzia leo.

Chama hicho kimekumbwa na mgogoro baada ya kuitisha uchaguzi lakini ukakataliwa na Ofisi ya Uchaguzi kwa maelezo kuwa haikuwa na taarifa.

Hata hivyo, ndani ya chama wapo wanaunga mkono uchaguzi wa Mwenyekiti wa Taifa, Aivan Maganza, na wengine wanampinga hivyo kusababisha kuwapo makundi yanayovutana baada ya uchaguzi huo uliofanyika  mwezi uliopita  Juni 29.

Makundi hayo ni lile linamuunga mkono makamu mwenyekiti wa chama hicho, Dominatha Rwechungura na katibu aliyeondolewa katika nafasi hiyo baada ya uchaguzi, Richard Lyimo. 

KUTEGUA KITENDAWILI

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, anasema mgogoro huo umeifikia ofisi yao.

Anafafanua kuwa wamepokea taarifa ya  uchaguzi huo kutoka kwa Makamu Mwenyekiti  TLP Taifa, Dominatha Rwechungura.

"Baada ya kuletewa taarifa za kufanyika uchaguzi wa mwenyekiti wa TLP taifa, tuliwasiliana na katibu mkuu wa chama, Richard Lyimo  kupata maelezo zaidi kuhusu uchaguzi," anasema Nyahoza.

Nyahoza anafafanua kuwa Lyimo aliwaambia kwamba hana taarifa yoyote kuhusu chama kufanya uchaguzi.

"Baada ya majibu hayo, tumemwandikia katibu huyo barua atoe maelezo kwa nini upande mmoja unasema uchaguzi ilifanyika na mwingine unakana kufanyika uchaguzi," anasema.

Anasema, Lyimo anatakiwa kupeleka maelezo haraka ili leo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itoe majibu ya hatima ya mgogoro wa kiuongozi ambao umejitokeza ndani ya chama hicho.

Anasema, kwa kawaida chama kinapomaliza kufanya uchaguzi, ni lazima kipeleke taarifa katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ili kupitia taarifa za uchaguzi huo.

"Hao walifanya uchaguzi wameleta taarifa zao tuzipitie tujiridhishe kwanza ili kuepusha migogoro ya kiuongozi ndani ya vyama," anasema. 

M/KITI APIGWA STOP

Tangu kufanyika kwa uchaguzi huo uliompa ushindi Aivan Maganza, mwenyekiti huyo mpya wa TLP hajaingia ofisini kutokana na kile anachoeleza kuwa ni kuzuiwa na walinzi wa makao makuu ya chama hicho.

Maganza anasema, baada ya kumalizika uchaguzi, Julai mosi aliripoti ofisini akiwa na safu mpya ya uongozi, akiwamo katibu mkuu mpya Riziki Ngaga.

"Lakini tulipofika tulizuiliwa na walinzi kwa maelekezo ya Lyimo na hadi sasa tumeshindwa kufanya kazi za chama kwa sababu ya mtu mmoja anayevuruga mambo," anadai Maganza.

Anasema, Lyimo alipata nguvu baada ya kuwapo taarifa kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haitambui uchaguzi huo, na kwamba walipeleka vielelezo vyote vya uhalali wa uchaguzi katika Ofisi ya Msajili.

"Kwa kuwa ofisi hiyo imepokea vielelezo, tunaamini itatenda haki katika maamuzi yake, kwa sababu hatukufanya uchaguzi kwa kificho, ofisi ya msajili inajua, Jeshi la Polisi linajua, ndio maana lililinda uchaguzi wetu," anasema.

KICHENI PATI

Akizungumzia tuhuma zinazoelekezwa kwake, Lyimo anasema, ni kweli amewazuia wasiingie ofisini, kwa maelezo kwamba chama hakijafanya uchaguzi.

"Kilichofanyika ni 'kicheni pati' sio uchaguzi, kwa sababu uchaguzi hauwezi kufanywa na wajumbe tisa. Hao ni wahuni tu," anasema Lyimo.

Anaongeza kuwa uchaguzi kama huo ni lazima katibu mkuu na kaimu mwenyekiti wa chama taifa wawepo, na kwamba yeye na kaimu mwenyekiti hawakuwapo.

"Kwa hiyo nirudie kusema kuwa hao watu walifanya 'kicheni pati' sio uchaguzi, kwa hiyo hatuwatambui kama viongozi bali ni wahuni tu," anasema.

UCHAGUZI ULIVYOKUWA

Katika uchaguzi huo, wajumbe wa mkutano mkuu walimchagua Maganza kuwa mwenyekiti wa chama hicho taifa kwa kura 35, huku Stanley Ndamugoba alipata kura 10, Kinanzaro Mwanga kura 10, Abuu Changaa kura sifuri na Richard Lyimo kura sifuri.

Hayo ni kwa mujibu wa makamu mwenyekiti wa chama, Dominatha Rwechungura ambaye anafafanua kuwa baada ya uchaguzi, halmashauri ilimchagua Riziki Ngaga kuchukua nafasi ya Lyimo aliyeondolewa katika nafasi hiyo na kubaki mwanachama wa kawaida.

"Lakini mwanasiasa mkongwe Hamad Tao, alichaguliwa naibu katibu wa chama chetu. Hao ndio baadhi ya viongozi wa juu wa TLP," anasema.

Uchaguzi huo ulifanyika baada ya kuahirishwa kwa zaidi ya mwaka mmoja huku ikielezwa kuwa chanzo cha hayo ni baadhi ya viongozi kung'ang'ania madaraka.

Mara ya kwanza, chama kilipanga kufanya uchaguzi Januari 8 mwaka jana, lakini ukaahirishwa hadi Machi 6, lakini haukufanyika ukapanguliwa hadi Mei mosi mwaka huo wa 2023.

Hata hivyo, uchaguzi huo pia haukufanyika ukasogezwa mbele hadi Desemba 28 mwaka jana, lakini ukaahirishwa ukapangwa kufanyika Januari 28, mwaka huu, nao ukapigwa kalenda.

Baada ya panga pangua hiyo, hatimaye ukafanyika Juni 29, lakini ili kuziba nafasi ilioachwa na Augustine Mrema aliyefariki dunia Agosti mwaka 2022,  lakini nao umekumbwa na sintofahamu baada viongozi waliochaguliwa kuzuiwa kuingia ofisini.