MAZINGIRA NA ELIMU: Athari za mfumo wa elimu kwa maendeleo ya akili ya watoto

By Dk. Felician Kilahama , Nipashe
Published at 11:26 AM Oct 22 2024
Mazingira rafiki ya kujifunzia ni ufunguo wa wasomi mahiri.
PICHA: MTANDAO
Mazingira rafiki ya kujifunzia ni ufunguo wa wasomi mahiri.

BINADAMU wote ni sawa lakini akili zinajengwa na kuimarishwa kulingana na mahali wanapoishi na mazingira yanayowazunguka.

Mathalani, mtoto anayezaliwa katika taifa lenye maendeleo makubwa, ni tofauti na anayezaliwa kwenye maendeleo kidogo, ukuaji na uendelezaji akili zao, kwa kiasi utatofautiana. 

Tunajiuliza, iweje tutofautiane kiakili kadri tunavyoendelea kukua hadi kuwa watu wazima? Ni kweli kuna kutofautiana katika kukua na kuendeleza akili kutegemeana na mambo kadhaa kama chakula na  uhalisia wa mazingira tuliyomo. 

Vilevile, jinsi tunavyolelewa pamoja na maneno tunayotamkiwa na wazazi au walezi na jamii akili za watoto zinaathirika.

Tunatafakari unapofika umri wa kuanza shule mtoto  anakuwa yupo vipi akilini? Anakwenda shuleni akibeba masuala gani akilini mwake? Walimu wanaompokea kiakili na kimaadili wakoje, wamepikwa kulingana na mahitaji ya jamii na taifa? 

Ni nini matarajio ya wazazi na walezi na taifa kwa watoto wanapokuwa shuleni kujifunza ? Je, katika mifumo ya maisha ya usasa tunatarajia elimu au mafunzo shuleni yatawawezesha kuwa bora kimaisha katika jamii?

Watakuwa wakulima, wafugaji na wafanyakazi werevu wanaotoa huduma bora au ni borahuduma? Sayansi ya jamii inaonyesha kuwa mazingira yanayomzunguka mtu humuunda kiakili na kitabia. 

Iwapo wanazaliwa na kukulia katika mazingira yenye ulevi uliokithiri, fujo na uovu mwingi, itakuwa vigumu kujengeka kiakili na kuwa wenye tabia nzuri. Kiuhalisia wakilelewa kwenye mazingira yaliyosheheni sauti zenye maneno na vitendo viovu watakengeuka. 

Kwa upande mwingine, tunapokuwa kwenye mifumo rasmi ya elimu; ndiyo wakati muafaka wa kujijengea msingi bora na imara kwa maisha ya utu uzima ili tusichanganyike kwani ni binadamu wenye karama tofauti.

Wakati wa uhuru 1961,  taifa lilitumia mfumo ya elimu wa  Waingereza,  baadaye liliweka mifumo iliyojengeka yenye maudhui tofauti. 

Mathalani, kwa kuzingatia miongozo: uhuru na kazi, ujamaa na kujitegema, binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja. Vilevile, kwa dhana ya binadamu ni utu hivyo, thamani kubwa ya binadamu ni kuuheshimu utu wake. 

Kutokana na mitazamo hiyo na masuala mengineyo kama nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko au sitapokea wala kutoa rushwa. Maudhui hayo yalijengeka kwa msingi kwamba haki ya mtu haiuzwi wala kununuliwa kwa chochote.  

Kwa kuyazingatia hayo taifa likajijengea mifumo ya elimu inayoendana na mazingira halisi, hata hivyo, ukafika wakati darasa la nane likafutwa,  na ilipofika 1967 ukaanzishwa mfumo wa elimu ya msingi mwisho darasa la saba.

Juhudi za kupanua elimu ya juu ziliendelea kiasi cha kufikia hatua ya kuona vyuo vilivyokuwa vinatoa mafunzo kwa ngazi za cheti  (astashahada) na stashahada (diploma)  kuwa vyuo vikuu. 

Vyuo vilikuwa vinatoa mafundi stadi mahiri kutokana na mafunzo au ujuzi alioupata mhitimu katika fani au mafunzo husika. Mathalani, mafundi umeme, mitambo, uashi na uhunzi. 

Sidhani kama kuwapo VETA sasa  ni toshelezi bado kuna haja kubwa kuwapo vyuo vya kati katika mifumo ya elimu na kuwajengea uwezo Watanzania.

     Serikali imedhamiria kuondoa elimu ya msingi kuishia darasa la saba ili na mfumo wa darasa la sita. Inawezekana pia ukafika wakati tukaamua kuwa elimu ya msingi imalizikie darasa la nne na kuendelea na sekondari hadi vyuo vikuu. 

     Kwa mageuzi kielimu ili kuwezesha vijana wengi kuyamudu maisha, kujiajiri au kuajiriwa wengine wanahitaji msingi imara. Hivyo, hatunabudi kuzingatia umuhimu na uwepo wa vyuo vya kati mahiri kwa vijana kupata mafunzo ya stadi za kazi, ngazi ya astashahada au stashahada kumwezesha mtaalamu kumudu kazi zenye kuhitaji maarifa fulani. 

Mathalani, kusimamia na kuendeleza shughuli mbalimbali kwenye vyama vya wakulima na ushirika vijijini pia mijini. 

Kadhalika, tunapotaka tushughulike na kilimo na ufugaji kibiashara na kuzingatia matumizi bora ya ardhi iliyotengwa kwa kilimo na ufugaji ni vyema wakulima na washauri elekezi wapatiwe mafunzo kikamilifu.

Uzoefu unaonyesha kuwapo ongezeko kubwa la wanafunzi tangu shule za msingi hadi vyuo vikuu, huku Watanzania wakizidi kuongezeka  lakini kwa upande mwingine taifa likoje kuuhalisia, kuhusu miundombinu kutoa elimu inayoikusudiwa? 

     Hali katika shule na vyuo si rafiki kwa mtoto au vijana wengi kupata elimu bora. Pamoja idadi yao kuendelea kuongezeka mikakati endelevu kuhakikisha miundombinu inaambatana na ongezeko la wanafunzi na wanavyuo, haijazingatiwa ipasavyo. Kwa utoaji elimu iliyo bora miundombinu inamaanisha madarasa, kumbi za mihadhara, vyumba vya maabara, ofisi za walimu na wahadhiri, vyoo toshelezi, majiko, mabwalo, kumbi za mikutano, stoo, nyumba za walimu na watumishi wengine, viwanja vya michezo na mafunzo kivitendo.

Wazazi na walezi tunawajibika kutembelea shule kuona mazingira yalivyo ili kubaini kama yanakidhi,  wanafunzi wanapata elimu bora. Watoto wanabanana kwenye madawati kukaa chini hadi kwenye miguu ya walimu, yaani kila mahali panajaa kiasi cha mwalimu kutowafikia wanafunzi nyuma ya darasa.

Je, ni sahihi? Siyo lakini hii ndiyo hali ilivyo kwenye shule zetu maana watoto wameongezeka wakati hakuna miundombinu ya kutosheleza. Iwapo hali iko hivyo kuna hatari ya kuwaona watoto wengi shuleni lakini hawafundishwi ipasavyo.

     Tanzania, inahitaji mifumo ya elimu mizuri kuwezesha vijana wote wapate elimu sahihi tangu msingi hadi vyuo vikuu. Ni jambo jema, lakini tumejiandaa vya kutosha na uhalisia wake ukoje? 

     Karibu vyuo vingi nchini vinadahili wanafunzi wengi na wanazuoni wanalazimika kufundisha watahiniwa 200 hadi 300 sehemu moja. Vilevile, hali halisi ilivyo kwa madarasa mengi shule za msingi namba ya walioandikishwa kuanza darasa la kwanza kwenye chumba kimoja chenye uwezo wa kutumiwa wanafunzi 45-50. 

     Namba hiyo humwezesha mwalimu kuimudu kazi yake barabara ikiwa ni pamoja na kutambua uwezo wa kila mwanafunzi kiasi cha kuwasaidia wenye uelewa hafifu ipasavyo. 

     Kwenye mijadiliano na baadhi ya wahadhiri  inaonekana ni vigumu kutoa mhadhara kwa watahiniwa waliojazana  sehemu moja wakaelewa . 

     Isitoshe baadhi ya waliosajiliwa kusomea shahada hawakidhi vigezo vinavyotakiwa hivyo hali hiyo inabaki kuwa kitendawili. Ukihoji mhadhiri kwamba unapotoa kazi ya kufanya kwa wanafunzi 200 hadi 300, unawezaje kusahihisha majibu yote kwa ufasaha na kwa kutenda haki? 

Majibu yanaonyesha kuwa ni vigumu kuyapitia kwa ufasaha inavyotakiwa. Wahadhiri kadhaa wanakiri kuwa hilo linawezekana kwa wahusika kati ya 50 mpaka 70 tu zaidi ni changamoto kubwa.  Hata hivyo wengi wanakiri kuwa namba muafaka ni wanafunzi 50 zaidi ya hapo ni kwenda kinyume na misingi kitaaluma. Inaelekea mmoja au wachache wakikamilisha kazi wenzake hupata majibu mitandaoni hivyo majibu karibu yanayofanana. 

     Nakumbuka nikisomea shahada ya kwanza miaka ya 1970s idadi ya watahiniwa ilikuwa  rafiki kwa wahadhiri kumudu majukumu kikamilifu. Somo la taaluma za maendeleo (development studies) linalohusu  wanafunzi karibu wote, lilichukua wanachuo kutoka fani mbalimbali, idadi ikawa kubwa  ikishangaza wahadhiri. 

Mmoja wa wahadhiri aliwahi kusema “namba yenu ni tishio hivyo ili niweze kukabiliana na changamoto hii, nalazimika kunywa angalau bia moja kujiweka sawa kabla ya mhadhara”.

 Pengine nia ya serikali ni kupata wataalamu wengi zaidi; wakati tukifanya hivyo tuwe makini ili  viwango visiwe chini kutokana na kutofautiana na mifumo vyuo vikuu. Vilevile, miundombinu kwenye vyuo iwe rafiki kuwezesha wanafunzi wengi wenye sifa zinazokubalika kusomea shahada. 

Kwa sasa halihalisi ya miundombinu si rafiki kutokana kumbi za mihadhara kuwa chache kuliko mahitaji. Kadhalika, maabara hazitoshelezi pia wakurufunzi na wahadhiri ni wachache. 

Zipo dalili zinazoashiria kuwa baadhi ya wahitimu vyuo vikuu, uwezo wa kumudu kazi au fani walizosomea ni wa chini kiasi cha kulazimika kupewa mafunzo kazini na au ‘kutemwa’ na mifumo iliyopo.

      Waajiri wanapenda wachapakazi mahiri siyo zaidi, hivyo nashauri ifanyike tathmini ya kina kuhusu mlundikano wanafunzi kwenye shuleni na vyuoni. Je, ni sahihi kuwepo mlundikano vyuo vikuu hususani tukizingatia mifumo na kanuni zilizowekwa ili kutoa elimu bora na siyo bora elimu.