Hadaa waganga matapeli, msanii aliyezikwa hai…2 Mama: Nilimwogopa, nawaza hata mimi pia angeweza kunitoa kafara kupata mafanikio

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 08:46 AM Sep 17 2024
 Rupia Boy
Picha: Nipashe Digital
Rupia Boy

ILIKUWA Desemba 20, mwaka 1996, Maria Asenga, alipata mtoto wake wa pili akampa jina la Salimu Mbasha maarufu Rupia, jina la usanii wa muziki.

Mama yake, anazungumzia tukio la kijana huyo kusaka mafanikio, hata kukubali kuzikwa akiwa hai mwaka 2022 katika juhudi za kupata utajiri bila kazi ngumu wala jasho.

Salimu au Rupia Boy (pichani), wiki iliyopita anaelezea mkasa huo, akisema baada ya kurekodi nyimbo kadhaa ambazo ni ‘odio’ (zisizokuwa video) lakini pia hazikupata mafanikio alipewa mbinu mpya za kumpaisha.

Akiwa kwenye moja ya studio Dar es Salaam anapata wanamuziki wanaomshauri kuwa atafanikiwa bila usumbufu kupitia mganga wakampa namba zake.

Anaahidiwa kuwa angempika hadi apate mafanikio makubwa kwa muda mfupi, hivyo hana haja ya kusumbuka. Jambo analolikubali.

Anawasiliana na mganga ambaye angemtajirisha kwa masharti kadhaa kuu likiwa kumlipa takribani Shilingi 700,000 na baada ya hapo angemzika na kumfukua akiwa mtu mpya kiutajiri na kimafanikio kwenye muziki bila nguvu wala jasho.

Rupia hakuwa na tatizo bila kujali kuwa hakuna mafanikio bila juhudi, akatapeliwa na kuzikwa hai, jambo ambalo bila jitihada za marafiki angeweza kupoteza maisha.

Mama yake mzazi, anazungumzia kisa hicho akisema ni jambo linalomshangaza mno:

“Nilimwambia kama unakubali kuzikwa hai kaburini, hata mimi mama yako unaweza kunitoa kafara ili kusaka mafanikio.” 

Rupia ni mtoto wa pili wa Maria Asenga, mkazi wa Tabata Kimanga, Dar es Salaam, anayemiliki mgahawa akiuza vyakula na vinywaji baada ya kuondoka Mwanga mkoani Kilimanjaro muda mrefu.

Anasema mtoto huyo amempata pamoja na mfanyabiashara wa madini Mererani (jina tunalo), na kwamba amelelewa na kutunzwa na familia yake na ya mwenza wake, kila mmoja akitamani asome.

Anasema, Rupia alipenda muziki tangu utotoni na kwamba akiwa Sekondari ya Kileo iliyoko Mwanga, anazama zaidi kwenye muziki.

“Namwambia mwanangu shika moja soma. Uko shule lakini umekwenda mitaani unaimba na kurekodi muziki kwanini usimalize masomo kwanza?” anasema Maria.

Anaongeza kuwa anaanza kurekodi ‘odio’  akiwa sekondari na kila siku hamu ya kuwa mwimbaji mkubwa inaongezeka rohoni mwake.

Anasimulia kuwa Rupia au Salimu hakumweleza kuhusu safari ya kwenda kwa mganga kusaka mafanikio, ila alishtuka kumwona akiwa taabani, baada ya kunusurika na kifo kilichotokana na mauzauza ya mganga.

“Nilishangaa kupata taarifa hizo kuwa amezikwa hai na ameokolewa na marafiki, anatibiwa na nikapaswa kugharamia matibabu.”

Anasema mshtuko huo umeathiri maisha yake kiasi cha kupata shinikizo la juu ya damu na kwamba kama angemweleza mpango huo angeukwamisha.

“Ilifika kipindi hata mimi namwogopa nawaza usalama wangu. Ni jambo lililonishtua mno.” anasema Maria.

Anaeleza kuwa baada ya kupata ushauri na mausia ya marafiki na ndugu, Rupia amebadilika na anaanza kuomba baraka za wazazi na bibi mzaa baba ambao wamemlea kabla ya kufanya jambo.

Anasema hana kipingamizi kwenye muziki maana ni kipaji chake na anaendelea kumsaidia.

Maria anaeleza kuwa anachomwomba Mungu ni kusahau mkasa huo na kumfanikisha kijana huyo kuendeleza kipaji chake. 

ALIYEMWOKOA

 Huyu ni Ali Khamis, rafiki wa karibu wa Rupia, anayesema ilishindikana kumshawishi na kumkataza Salimu kukubalina na mganga.

Anasema wamekuwa pamoja na kusoma Sekondari ya Kileo na kwenye mpango wa kusaka hela chap chap, alimshauri aachane nao.

“Nilimshauri sikueleweka. Alikutana na watu wenye ushuhuda jinsi walivyofanikiwa na wakawa na nguvu kubwa ya ushawishi,” anasema Khamis.

Anaeleza kuwa walikuwa pamoja hata alipoambiwa kuwa atazikwa hai, jambo lililomstua sana, akamkataza.

Anakumbusha kuwa walielekea Iringa pamoja na kufahamu alipopelekwa na kufanyiwa uganga huo, ambao anasema hakuuamini hata kidogo.

“Tuliambiwa atazikwa kwa muda. Nilishangaa mbona hakuna uhusiano? Utajiri na kuzikwa hai unahusianaje? Lakini tukazidi kujiuliza hayo ndiyo masharti mbona ni ajabu?”

Khamis ambaye wakati huo, alikuwa karibu zaidi na Rupia, hakumwacha aende Iringa peke yake aliambatana naye hadi porini na kushuhudia kilichoendelea akaazimia kuchukua hatua.

“Kwanza niliwaza kufukiwa ardhini kutasababisha kukosa hewa na kuzimia hata kupoteza maisha.” Anasema Khamis ambaye sasa ni askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, akiwa kazini mkoani Tabora.

Anaeleza kuwa walimsaka mganga kwa simu kujua lini anamfukua, maana masharti hayo yalikuwa adhabu kwa ndugu yao, lakini hakupatikana kwa simu.

Anasema baada ya kuona wamepigwa changa la macho, walimfukua akiwa taabani asiyejitambua na kumkimbiza hospitalini.

“Huko nako tuliona kazi itakuwa ngumu maana mtu hajielewi, kusema alizikwa hai ingekuwa kesi nyingine. Hatuna fomu ya polisi namba tatu (PF3) hilo lilitatiza lakini tulikwenda kwenye hospitali binafsi kuomba huduma,” anasema Khamis.

Anakumbuka kuwa wakiwa hospitalini walimfikisha kama jamaa ambaye wanakutana mitaani lakini safari hiyo hali yake ilishangaza marafiki zake wakalazimika kumfikisha hospitalini.

ANA USHAURI

Khamis anawataka vijana na yeyote anayetamani mafanikio afanye jitihada zaidi atumie mbinu bora na akili zaidi.

“Kupata maisha bora ghafla si rahisi. Ni kitu kigumu. Watu wakumbuke kuwa fedha au utajiri si mvua, jua au nguvu nyingine za asili. Tuongeze juhudi zaidi,” anasema Khamis.

Aidha, anasema haiwezekani mtu wa kawaida akawa mfanyabiashara mkubwa ghafla akimiliki mfano mabasi ya mikoani bila kuanza na bodaboda, bajaji na daladala, akimaanisha kuwa ni lazima kupitia hatua ili kupanda juu zaidi.

“Jingine kubwa tusiamini na kupokea ushauri hasa wa watu ambao hatuwafahamu. Usikutane na mara moja na jamaa akakushauri ukamwamini. Hapana, akili au ushauri unaopewa changanya na wako.” 

Anaeleza kuwa watu waepuke kuamini shuhuda ambazo wakati mwingine si za kweli maana wengi wamepotelea au kuangamia kwa kupokea maelezo ambayo hayathibitishwi.

 KISA KILIVYOKUWA.

Rupia akielezea mkasa huo uliochapishwa wiki iliyopita anasema, baada ya kufanya mawasiliano, alikutana na mganga huyo Sinza kwenye eneo la burudani.

Baada ya majadiliano na kulipa waliondoka Dar es Salaam kwenda Iringa kwenye msitu asioufahamu. 

“Tuliondoka usiku mganga akiendesha gari lake binafsi. Tulifika sehemu hiyo akanionesha jeneza na kila kitu kilikuwa kimeandaliwa.” Anasema Rupia.

Anaeleza kuwa, mganga alikuwa amewasiliana wa wenyeji wao na ilikuwa ni kufika na ‘kutibiwa’ au kufukiwa.

Anasema kabla ya kuingia kwenye jeneza la mbao, alichomwa sindano kwenye mshipa mkuu wa mkono wa kushoto, akapoteza fahamu.

Mganga alimwahidi kufukua baada ya siku mbili, na kwamba alifukiwa Ijumaa saa 9 usiku hivyo, angemfukua tena Jumapili saa 9 usiku pia.

Rupia, anasema aliingiwa na wasiwasi, katika safari hiyo aliyokuwa ameambatana na marafiki zake, akiwaambia, ikifika wakati huo kama mganga hajamfukua, wamfukue na iwapo atafariki au atapata shida yoyote wamwambie mama yake na hicho ndicho Ali Khamis alichokifanya.