ZAIDI ya watoto 30 waliofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia wanalelewa katika vituo vya watoto yatima vilivyopo Manispaa ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Watoto hao, ambao wamepitia mateso, wakiwemo waliobakwa na kupigwa na wazazi au walezi wao, sasa wanapatiwa huduma na wasamaria wema kupitia uongozi wa Serikali za Mitaa na Ustawi wa Jamii.
Kikundi cha Wajomba Family cha Kigamboni, kimechanga fedha ili kununua mahitaji muhimu kwa watoto hao, ili kusherehea sikukuu ya kuvuka mwaka.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Wajomba Family, Salum Ally Ramadhan, amesema kuwa wameamua kusaidia watoto yatima kutokana na mazingira magumu wanayoishi.
“Kila mwaka tunachangishana fedha na kutoa misaada ya vyakula, nguo, mafuta ya kupikia, maji ya kunywa, na mahitaji mengine muhimu. Kigamboni kuna vituo 10 vya watoto yatima, na tunapanga kuvifikia vyote na kuhakikisha wanapata huduma zinazohitajika,” alisema Ramadhan.
Katika kufunga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka 2025, Kikundi cha Wajomba Family kimetoa misaada kwa vituo sita vya watoto yatima.
Amesema msaada huo unajumuisha chakula, mafuta ya kupakaa, mafuta ya kula, maji ya kunywa, na nguo, ili watoto hao nao waweza kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya kwa furaha, kama watoto wengine.
Katika kusherehekea sikukuu yam waka mpya, Ramadhan, amewaomba wazazi na walezi kuacha migogoro isiyokuwa na msingi ndani ya ndoa, kwani migogoro hiyo ni chanzo kusababisha ukatili wa kijinsia kwa watoto na kuishia kulelewa katika vituo.
Ameongeza kuwa, ili kudhibiti hali hiyo, ni muhimu Serikali isimamie sheria ya ndoa ya mwaka 2019 na sheria ya mtoto ya mwaka 2009 kwa kuhakikisha haki za watoto zinaheshimiwa.
Mlezi wa Kituo cha Hisani Orphanage Centre kilichopo Kibada, wilayani Kigamboni, Moza Omary, amesema kuwa kituo hicho kinahudumia watoto 84, kati yao wasichana 52 na wavulana 32.
Amesema watoto hao ni wale waliokumbwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia, waliotoka katika familia maskini, na wengine ambao wamefiwa na wazazi wao.
Vilevile, Msimamizi wa Kituo cha Yerusalem, Elizabeth Moses, ameeleza kuwa wanahudumia watoto 32, wakiwemo wale waliotoka katika mazingira hatarishi na wale walioathirika na ukatili wa kijinsia.
Mlezi wa Kituo cha Amani, Sauda Hashim Juma, ameongeza kuwa wanahudumia watoto 56, kati yao wasichana 30 na wavulana 26, ambao pia ni yatima na waliokumbwa na mateso.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Maweni, Kata ya Mawenzi, Said Mzuwanda, ameomba wadau wengine kuiga mfano wa Kikundi cha Wajomba Family katika kusaidia watoto wenye mahitaji maalum.
Amehimiza kuwa msaada wa aina hiyo ni sadaka inayompendeza Mungu na inatoa baraka kutoka kwa watoto hao, ambao wangeweza kuwa na familia bora, lakini mazingira yamewafanya wapigane na changamoto kubwa za maisha.
Ameongeza kuwa, wataendelea kuunga mkono juhudi za Kikundi cha Wajomba Family kwa kuhakikisha wanatembelea vituo vya watoto yatima mara kwa mara na siyo tu wakati wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
Kwa upande mwingine, Shekhe Musa Omary aliiomba Wajomba Family kuwasaidia watoto hao kwa chakula na mavazi hasa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, kipindi ambacho mahitaji ya misaada huwa ni makubwa zaidi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED