Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza usaili wa ajira za kada ya ualimu ambazo awali usaili wao ulisitishwa kwa muda, utafanyika kuanzia Januari 14, 2025 hadi Februari 24, 2025.
Oktoba 17, 2024, Ofisi hiyo ilitangaza kusitisha usaili huo wa nafasi za kazi za walimu wa shule za msingi na sekondari zaidi ya 11,000 zilizotangazwa Julai, 2024 ambazo waombaji maelfu walikuwa wameitwa kwenye tangazo lililotolewa Oktoba 15, 2024.
Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi hiyo iliyotolewa Desemba 31, 2024 na kusainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini wa ofisi hiyo, Lynn Chawala, Katibu wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma anapenda kuwatangazia waombaji kazi wote wa kada ya ualimu ambao usaili wao ulisitishwa kwa muda, usaili huo utafanyika kuanzia Januari 14, 2025 mpaka Februari 2025.
Vile vile, "Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma anawajulisha wasailiwa wote wa kada za ualimu kuwa, usaili wa kuandika (mchujo) na mahojiano ya ana kwa ana utafanyika ndani ya mikoa wanayoishi wasailiwa na watapangiwa vituo vya kazi kulingana na ufaulu wao popote nchini." Ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED