Mzazi aanika risasi iliyoua mwanafunzi

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 07:05 AM Sep 14 2024
Mzazi aanika risasi iliyoua mwanafunzi
Picha: Mtandao
Mzazi aanika risasi iliyoua mwanafunzi

RISASI iliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Lulembele, Teresia John (18), ambaye alifariki dunia wakati wa vurugu na maandamano ya wananchi katika Kituo cha Polisi Lulembela, wilayani Mbogwe, mkoani Geita, ilipitia dirishani, imeelezwa.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Grace Wilson, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofika nyumbani kwake kufuatilia tukio hilo.

Mauaji hayo yalitokea Jumatano ya wiki hii wakati wananchi wakitaka kuwashambulia na kuwaua watu wawili waliotuhumiwa kuiba mtoto.

Grace alisema risasi hiyo ilipitia dirishani na kupasua kioo kisha kumpata mtoto wake aliyekuwa chumbani muda mfupi baada ya kuwataka waingie ndani kuepuka vurugu hizo.

“Alikuwa chumbani nilishtuka anakuja anakimbia sebuleni tulipokuwa sisi, alifika akaniangukia kifuani na kupoteza maisha hapo hapo. Nivyomwangalia kifuani damu zilikuwa zinatoka, niliona tundu limetokea mgongoni,” alisimulia mama huyo.

Grace kabla ya tukio hilo mtoto wake, alikwenda kwa fundi kujaribisha nguo aliyotakiwa kuivaa katika sherehe ya dini.  Aliporudi vurugu zilikuwa zimeanza, hivyo akatutaka tuingie ndani na yeye akaingia chumbani ambako tukio hilo lilimkuta.

MTENDAJI AFUNGUKA

Mtendaji wa Kata ya Lulembela, Frank Gonja, alisema wakati  tukio hilo linatokea kulikuwa na gulio na watu walikuwa wengi.

“Baada ya kuwaona vijana hao waliobeba watoto, mmoja akiwa hana nguo walianza kushambuliwa. Hisia ziliwatuma kuwa ni miongoni mwa matukio ya wizi wa watoto, hivyo hawakutaka kujiridhisha, wakaamua kuwashambulia, walikuwapo watendaji wa vijiji, lakini walipotaka kusaidia hali ilikuwa mbaya zaidi,” alisema Gonja.

Alisema alipokea taarifa kuwapo kwa vurugu hizo, hivyo kuelekea katika eneo la tukio akiwa na pikipiki ambako alifanikiwa kuwabeba vijana hao ambao walikuwa na watoto na kuwapeleka katika kituo cha polisi ambako pia wananchi waliwafuatilia nyuma.

Baada  ya kuwafikisha kituoni, alisema waliwahoji na kubaini kuwa watoto wale ni wa mmoja wao na walijihakikishia kwa kuwasiliana kwa simu na mama yake ambaye alithibitisha kwa majina ya watoto hao kisha kufika kituoni na watoto kumtambua.

“Wananchi walijulishwa lakini hata hivyo hawakutaka kuelewa na kuendelea na vurugu na ndipo walipoomba msaada wa askari kutoka wilayani na mkoani, ambao walisaidia kutuliza vurugu hizo na ikatambulika kuwa kuna watu wawili wamefariki dunia,” alisema Mtendaji huyo.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo akiwamo Mary Peter, alisimulia kuwa baada ya vurugu hizo yeye na watoto wake walijificha uvunguni mwa kitanda kujinusuru.

TUME YALAANI 

Kutokana na tukio hilo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, imelaani kitendo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, amewataka wananchi kuwa wavumilivu na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria katika kukabiliana na masuala ya namna hiyo.