Muuzaji wa jumla, tani 1.8 zanaswa

By Zanura Mollel ,, Grace Gurisha , Nipashe
Published at 10:52 AM Sep 11 2024
 Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
Picha: Mtandao
Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imetangaza kumkamata inayemtaja kuwa mfanyabiashara wa jumla wa dawa za kulevya nchini.

Mtuhumiwa huyo, Richard Mwanri (47), mkazi wa Mbezi Makonde, wilayani Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, anadaiwa ndiye msambazaji mkuu wa dawa hizo nchini. 

"Richard ni mhalifu ambaye amekuwa anapokea dawa za kulevya kutoka nchi mbalimbali na kuingiza nchini kwa usafiri wa magari zikiwa zimefichwa kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine kisha kusambazwa kwa wauzaji wengine katika maeneo mbalimbali nchini," amesema Kamishna Jenerali Aretas Lyimo. 

Ni alipozungumza na vyombo vya habari jijini jana kuhusu operesheni iliyofanyika kuanzia mwezi uliopita hadi Septemba 2 mwaka huu mkoani Dar es Salaam. 

Alisema kuwa katika operesheni hiyo, walikamata kilogramu 1,815 za bangi iliyosindikwa, maarufu skanka. 

Pia walikamata watuhumiwa watano wanaohusishwa na dawa hizo, wakiwamo Mwanri na Felista Mwanri (70) ambaye ni mmiliki wa nyumba ambayo inadaiwa dawa hizo zilikutwa. 

Watuhumiwa wengine ni Athumani Mohamed (58), mkazi wa Mkoa wa Tanga; Omary Mohamed (32), dereva bajaji na mkazi wa Buza, wilayani Temeke, Dar es Salaam; na Juma Chapa (36), mkazi wa Kiwalani, Dar es Salaam. 

Kamishna Jenerali Lyimo alisema kuwa dawa hizo zilikamatwa katika maeneo mbalimbali mkoani hapa, yakiwamo Luguruni, Mbezi na Magomeni. 

Kwa mujibu wa DCEA, skanka ni miongoni mwa dawa za kulevya inayotajwa kuwa na kiwango kikubwa cha kemikali zenye sumu aina ya Tetrahydrocannabinol (THC) na huleta athari kwenye mfumo wa fahamu.

 "(Skanka) pia huleta matatizo ya akili pamoja na kusababisha magonjwa yasiyoambukiza kama vile maradhi ya moyo, figo na ini. Matumizi ya skanka kwa wajawazito yanaweza kuleta madhara kwa mtoto aliyeko tumboni, ikiwamo kuathiri mfumo wa ubongo na kuzaliwa na uzito mdogo," alisema Kamishna Jenerali Lyimo. 

Kamishna Jenerali Lyimo pia alisema kuwa katika operesheni hiyo, walikamata gari aina ya Mitsubishi Pajero lenye namba za usajili T 551 CAB na bajaji yenye namba za usajili MC 844 CZV.

 Alirejea taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Duniani iliyotolewa Vienna, Australia mwaka huu, ikionesha kuwa maeneo yaliyohalalisha matumizi ya bangi, yanashuhudiwa kuwa na uzalishaji bidhaa za bangi zenye kiwango kikubwa cha kemikali THC. 

Kamishna Jenerali Lyimo alisema taarifa hiyo pia imeonesha kuwa nchi zilizohalilisha matumizi ya bangi, zimekuwa na ongezeko la watu wanaohitaji tiba kutokana na matumizi ya bangi sambamba na ongezeka la watu wenye matatizo ya akili na waliojaribu kujiua.

"Mamlaka ipo katika mchakato wa kuvunja mtandao mkubwa wa dawa za kulevya nchini, dawa hizi zinatishia maisha ya watu.

 "Pia niombe wamiliki wa nyumba muwe makini na aina ya mzigo mnayopokea katika nyumba zenu," alihadharisha Kamishna Jenerali Lyimo.

MAHAKAMANI

Muda mfupi baada ya DCEA kutoa taarifa hiyo, bibi wa miaka 70, Felista Mwanri na mwanawe huyo, Richard (47) na watu wengine watatu walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mashtaka ya kusafirisha zaidi ya tani moja ya bangi.

 Mshtakiwa Richard alidai mahakamani kuwa mama yake huyo hahusiki, hivyo aachiwe huru; hali ya bibi huyo kwa mwonekano haikuwa nzuri, akisaidiwa kutembea.

 Washtakiwa wengine ni Mohamed, maarufu Makame (58) Chapa (36) na Omary (32), waliotajwa awali na DCEA.

 Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Eric Davis alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Godfrey Mhini kuwa washtakiwa hao wanatuhumiwa kwa shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha sheria.

 Alidai kuwa washtakiwa wanatuhumiwa kuwa Agosti 28 mwaka huu, wakiwa eneo la Tairo Luguruni, barabara ya Kwembe, ndani ya Wilaya ya Ubungo walikutwa wanasafirisha dawa za kulevya aina ya bangi kilogramu 1,815.

 Kuhusu hatua ya upelelezi ilipofikia, Wakili Davis alidai kuwa haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo.

 Kuhusu ombi la kuachiwa huru kwa mshtakiwa wa pili, Hakimu Mhini alimweleza mshtakiwa Richard kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

 Hakimu Mhini aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 24 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na kuangalia hatua ya upelelezi ilipofikia.