Mavunde apiga ‘stop’ uchimbaji madini Mto Zila

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:13 PM Dec 31 2024
Mavunde apiga ‘stop’ uchimbaji madini Mto Zila
Picha:Mpigapicha Wetu
Mavunde apiga ‘stop’ uchimbaji madini Mto Zila

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amesimamisha uchimbaji madini ya dhahabu kwenye Mto Zila hadi wataalamu wa mazingira watakapothibitisha kama hakuna madhara.

Alitoa msimamo huo jana kwa kusitisha shughuli hizo zinazofanywa na kampuni ya G & I Tech. Mining Company Ltd kwa kipindi hiki cha mvua za masika. 

Awali, Mavunde alitembelea eneo la leseni ya mwekezaji huyo lililoko kijiji cha Ifumbo lililovamiwa na wananchi na kusababisha mgogoro na uharibifu wa mali.

"Tumetembelea maeneo yote mawili na sote tumejionea hali halisi ya mazingira. Ni dhamira na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuona shughuli zote za kiuchumi hususani za madini zinafanyika kwa utulivu bila kuleta migogoro na pasipo kuathiri mazingira ya eneo shughuli zinapofanyika,” alisema,

 Mavunde alisema amesikiliza hoja za wananchi juu ya uharibifu  wa mazingira huo, hivyo serikali itaunda timu ya wataalamu kufanya tathmini ya kina ya mazingira juu ya athari zinazoweza kutokea wakati wa uchimbaji wa madini.

Mavunde alisisitiza kuwa kwa sasa shughuli zote za uchimbaji madini zisimame kwa kipindi hiki cha mvua za masika kama Tume ya Taifa ya Kudhibiti Uharibifu wa Mazingira kutoka NEMC ilivyoelekeza.

Wakati Mavunde akitangaza uamuzi huo, wizara hiyo kwa kushirikiana na watalaamu wa mazingira na wananchi ilikuwa inakwenda kuunda timu ya pamoja ya kufanya tathmini ili iwaeleze kitaalamu iwapo shughuli za uchimbaji madini zinaweza kuendelea kufanyika pasipo athari kwenye mazingira katika mto huo.

“Nitumie fursa hii kuwataka wananchi wote kuacha vitendo vya uvunjifu wa amani na kujichukulia sheria mkononi, tunalaani kitendo cha kuvamia na kuharibu mali za mwekezaji,“ alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya,  Mbarak Batenga, alishukuru ujio wa Waziri Mavunde na kusisitiza utaleta suluhisho la kudumu la mgogoro baina ya mwekezaji na wakazi wa Kijiji cha Ifumbo.

Batenga alisema serikali ngazi ya wilaya itaendelea kusimamia sheria na kanuni ili kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama muda wote.

 Mbunge wa Chunya, Masache Kasaka, kwa niaba ya wananchi aliishukuru serikali kwa namna inavyoshughulikia changamoto zao.

Alisema ombi la wakazi hao ni kuona mazingira ya Mto Zila yanatunzwa kwa kuwa ni chanzo kikubwa cha maji kwa wilaya hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, alimshukuru Mavunde kwa kutembelea Chunya na kuahidi kusimamia maelekezo yake ya kuona shughuli za uchimbaji katika mto huo zinasimama kwa kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha.