Madereva 64 wa mabasi wafutiwa leseni

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 08:41 AM Jan 01 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Simon Maigwa.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Simon Maigwa.

MADEREVA 64 wa mabasi makubwa na madogo yanayotoa huduma za usafirishaji katika mkoa wa Kilimanjaro, wamefutiwa leseni kutokana na makosa ya mwendokasi, kusababisha ajali, ulevi na kuyapita magari mengine bila tahadhari.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Simon Maigwa, madereva wengi waliopoteza ajira zao ni waliosababisha ajali, kundi hilo likiwa na madereva 32 waliofutiwa leseni.

Alisema eneo lingine lililotikisa kwa makosa na kufutiwa leseni kati ya Januari hadi mwezi Desemba 2024, ni la madereva 22 waliokuwa wakitembea kwa mwendokasi.

Alisema madereva waliofutiwa leseni kwa sababu ya makosa ya kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa, ni watatu na waliokuwa wakivunja sheria za usalama barabarani kwa kuendesha na kuyapita magari mengine bila tahadhari (wrong overtaking), waliofutiwa leseni ni madereva saba.

Kuhusu matukio ya ukatili wa kijinsia kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, Kamanda Maigwa alisema makosa ya kubaka 42 yaliripotiwa. 

Alisema kuwa makosa ya ulawiti yaliyoripotiwa ni 18. Makosa mengine yaliyoripotiwa ni manne ya kuwapa mimba wanafunzi sawa na idadi ya makosa ya ukatili dhidi ya watoto, hivyo kufanya jumla ya makosa kuwa 68.

Kati ya makosa hayo ya ukatili wa kijinsia, washtakiwa katika kesi hizo wamepewa adhabu ya kifungo cha maisha na wengine miaka 30 gerezani.