MABALOZI wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani, wamehimizwa kutumia taaluma, uzoefu na ujuzi tofauti walionao ili kuharakisha mabadiliko ya kimfumo yanayoendelea ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka alipoongea na Mabalozi hao, katika warsha ya siku 4 ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya mambo ya nje, inayofanyika mjini Kibaha mkoani Pwani.
"Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mmebarikiwa kuwa na watu wenye taaluma tofauti na wenye historia ya sekta tofauti, tumieni fursa yenu hii kumsadia Mwanadiplomasia namba moja, Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amewarahisishia kazi yenu kwa kuitekeleza diplomasia kivitendo," Balozi Kusiluka amesema.
Amesema Serikali inazitambua changamoto wanazokabiliana nazo na inazifanyia kazi lakini kutokana na wizara kuwa na watu wenye uzoefu wa kutoka sekta tofauti, wakishirikiana wanaweza kuzitatua na kuifikisha nchi katika hatua nzuri.
Kiongozi huyo pia aliwapongeza Mabalozi kwa kazi nzuri wanayofanya na kuwaahidi kuwa Serikali itapokea mawazo yote mazuri na ya kibunifu na kuyafanyia kazi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED