JESHI la Polisi mkoani Mbeya,limepiga marufuku mtu yeyote kupiga au kulipua milipuko (Fataki) bila kuwa na kibali cha jeshi hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi(SACP) Benjamin Kuzaga, ametoa kauli hiyo leo baada ya kukagua doria ya ukakamavu kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama kwenye sikukuu ya kuvuka mwaka.
Amesema jeshi hilo, limejipanga vizuri kuhakikisha wananchi wanasheherea kwa amani na utulivu, sikukuu hiyo.
Kamanda huyo amesema wataimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ya Jiji la Mbeya kwa kutumia doria za magari, miguu na mbwa wa polisi.
“Tupo timamu kuhakikisha wananchi wanasheherekea sikukuu ya mwaka mpya kwa amani na utulivu na kuimarisha ulinzi katika nyumba za ibada na misa za mkesha, makanisani na misikitini,” amesema Kuzaga.
Ameongeza kuwa vikosi vya polisi vitakuwepo kwenye maeneo yote tete, barabara kuu, milima Iwambi, Igawilo na Mlima Nyoka ili kudhibiti ukiukwaji wa sheria za barabarani na kwamba wanavyo vifaa vya kupima mwendo kasi, ulevi na watakaobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Natoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuchoma matairi barabarani kwa kufanya hivyo ni kuharibu miundombinu iliyowekwa na serikali badala yake washerehekee kwa amani na utulivu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED