Jacob apata dhamana atoa mambo matano mazito

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:57 AM Oct 08 2024
Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Pwani, Boniphace Jacob (katikati), akifurahia pamoja mawakili wake, Dickson Matata (kushoto) na Peter Kibatala, baada ya kupata dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana.

ALIYEKUWA Meya wa Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob, maarufu kwa jina la ‘Boni Yai' ametaja mambo matano aliyojifunza akiwa mahabusu atakayokwenda kuyasimamia baada ya kutangazwa mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Pwani.

Akizungumza jana katika viunga vya Mahakama ya Kisutu baada ya kupata dhamana hiyo, alisema kukaa kwake gerezani kumemsaidia kuifahamu nchi, kwa kuwa alikutana na wafungwa waliomweleza matatizo yao.

Alisisitiza uzoefu alioupata anataka kuutumia katika kuendeleza mapambano yake kudai haki kwa Watanzania, hasa waliokosa fursa za kisheria.

Alisema kutokana na funzo alililopata atawalipia  wafungwa 10 faini wanazodaiwa katika Gereza la Segerea,  huku mmoja akiwa tayari amelipiwa faini  na wengine tisa wakikamilishiwa leo ili wawe huru.

Pia, aliahidi kuwatafutia mawakili na kulipa gharama, wafungwa 20 wa makosa mbalimbali, mengine yakiwa hayana dhamana katika gereza hilo.

Alisema ameamua kufanya hivyo baada ya kuwasikiliza na kubaini wanahitaji msaada wa mawakili wa jopo kama alilonalo, alidai tayari amechukua orodha yao na ataikabidhi kwa mawakili ili waanze kushughulikia.

Akizungumzia hali ya watu waliopotea au kutekwa, Jacob alisema kero hiyo lazima iishe, na kama itaendelea, yeye atakuwa mstari wa mbele kuendelea kupambana, hata kama atakwenda jela mara kwa mara.

USHINDI

Pamoja na changamoto za kuwa gerezani, Jacob aliibuka mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani ya CHADEMA katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 5.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Kibaha, mkoani Pwani, alipata kura 60 sawa na asilimia 77, akimshinda mpinzani wake Gervas Lyenda, aliyepata kura 17.

Akiwa mwenye furaha kwa ushindi huo, Jacob alisema wanachama wa CHADEMA wamempa deni la utumishi kwa miaka mitano ijayo, atahakikisha Kanda ya Pwani inakuwa yenye heshima, haki, na usawa.

Alisema atahakikisha kuwapo kwa usawa wa kisiasa na haki za jinai, huku akikazia umuhimu wa kuunganisha vijana waliosoma sheria na hawana ajira kunufaika na eneo la haki jinai ambao litakusanya watu wa kada hiyo ili kuwasaidia wananchi kupata haki zao.

MNYIKA

Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alipongeza uamuzi wa kumpa Boniface dhamana kwa kuwa hakukuwa na haja ya msingi ya kumnyima haki hiyo.

Aidha, alisema kutoka kwake kwa dhamana hakumfanyi kuwa huru kwa kuwa bado ana kesi inayoendelea na kuiomba Jamhuri ipeleke hati ya kutokuendelea na kesi hiyo kwa kuwa anaona haina mashiko.

MAHAKAMANI

Jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilimpa dhamana Boniface baada ya kusota rumande kwa siku 19 kutokana na pingamizi la dhamana lililowasilishwa na jopo la mawakili wa Jamhuri.

Alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Septemba 19, 2024 akituhumiwa kwa mashtaka mawili likiwamo la kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii.

Upande wa Jamhuri uliwasilisha pingamizi la Jacob kutopewa dhamana kwa madai ya usalama wake, kabla ya kutolewa kwa uamuzi wa pingamizi hizo, Jamhuri iliwasilisha tena maombi mengine mapya ya kiapo cha ziada katika kesi hiyo.

Akitoa uamuzi huo mdogo, Hakimu Kiswaga alisema, kiapo cha RCO wa Mkoa wa Polisi Kinondoni, Davis Msangi hakina maelezo ya ziada ya kutosha kuzuia dhamana hiyo.

Alisema sababu zilizotolewa hazina maelezo ya ziada ya kwanini mahakama isitoe dhamana, kwamba iwapo mjibu maombi ametoa maelezo ya usalama wake alitegemea mwombaji (Jamhuri) kupeleka uthibitisho wa maelezo ya mjibu maombi (Jacob).

Kutokana na hali hiyo, Mahakama ilikubaliana na maombi ya utetezi, mjibu maombi atapewa dhamana kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa na mahakama hiyo, kwa hiyo inatupilia mbali pingamizi la upande wa Jamhuri la kuzuia dhamana.

Hakimu Kiswaga alisema ili mshtakiwa awe nje ya dhamana anatakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua za Serikali za Mitaa na pia watatia saini bondi ya Shilingi milioni saba kila mmoja.

Hata hivyo, Jacob ametakiwa asitoke nje ya nchi bila kibali cha mahakama na ametimiza masharti hayo na kuachiwa huru. Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 21, 2024 kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika.

Kabla ya kutolewa uamuzi huo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema, alidai mahakamani kuwa wana maombi madogo yasikilizwe kwanza kabla ya uamuzi.

Hata hivyo, Wakili wa Jacob, Peter Kibatala alipinga hoja hiyo na kuiomba mahakama isikubali kuendeshwa na watu ambao hawajazingatia taaluma.

Baada ya hoja hizo, Hakimu Kiswaga alikataa hoja hiyo ya Mrema na kusema kuwa dhamana ni haki ya kikatiba ya mtu kupewa, wasubiri kwanza atoe uamuzi kama wana hoja zingine basi zije baadaye.

Jacob, anatuhumiwa kwa mashtaka mawili likiwamo la kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wake wa kijamii.

*Imeandikwa na Grace Gurisha na Grace Mwakalinga