Dk. Nchimbi atoa siku 27 wanafunzi kulipwa 'boom'

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 05:31 PM Jun 04 2024
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk.Emmanuel Nchimbi.
Picha: Romana Mallya.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk.Emmanuel Nchimbi.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk.Emmanuel Nchimbi, amempa muda hadi mwishoni mwa mwezi huu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, kumaliza tatizo la fedha za kujikimu (Boom) kwa wanafunzi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Tengeru, ambao wana miezi sita hawajapata.

Agizo hilo limetolewa  leo baada ya Mwanafunzi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Tengeru, mkoani Arusha, Digna Nasari, ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa CCM Kata ya Ambureni, kumweleza katibu mkuu huyo kuwa mpaka sasa ni mwezi wa sita wanachuo chuoni hapo hawajapata 'Boom'.

Akizungumza na wananchi wa USA-River, Wilaya ya Meru, mkoani hapa, Balozi Nchimbi ambaye amehitimisha ziara yake Arusha na kuelekea Mkoa wa Kilimanjaro, amemwelekeza Waziri wa Elimu kwamba, tatizo hilo liishie ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.