Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linamsaka Mwita Yoba, kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba na kusababisha vifo vya watu wanne, ambao ni mama na watoto wake watatu.
Akizungumza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, amesema tukio hilo limetokea Desemba 30 mwaka huu saa 10:45 alfajiri katika Kitongoji cha Kwedichocho ,Kijiji cha Manga Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Amewataja waliofariki kuwa ni Pili Saguge(28),mkulima na mkazi wa Kwedichocho (mama), Chacha Nyabilenga, Jane Nyabilenga na Makabala Nyabilenga.
Aidha Kamanda huyo amesema kwamba baada ya kufanya tukio hilo mtuhumiwa alitoroka na kutokomea kusikojulikana.
Kamanda Mchunguzi amesema chanzo cha mauaji hayo ni mtuhumiwa kuishtumu familia hiyo kwa madai ya kumuua mtoto wake kwa sumu hali iliyomsukuma kutekeleza mauaji hayo kwa kulipiza kisasi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED