Adaiwa kumuua mtoto wa kufikia, abeba sehemu za siri, viganja

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 07:52 PM Jun 04 2024
Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama
Picha: Maktaba
Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama

HATIMAYE Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limefanikiwa kumkamata Erick Julias (39) mkazi wa Mlimba, mkoani Morogoro, kwa tuhuma za kumuua kwa kumtenganisha kichwa pamoja na viungo, mtoto wake wa kufikia aitwaye Johnson Ngonyani (6) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya awali.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema pamoja na mtuhumiwa huyo kudaiwa kumkatakata viungo mtoto huyo, pia inadaiwa kuwa alikata sehemu za siri pamoja na viganja vya mtoto huyo, kisha kuondoka navyo.

Kamanda Mkama amesema mtuhumiwa alitenda ukatili huo Juni 1 mwaka huu majira ya usiku huko katika Kitongoji cha Kigamboni, Kijiji cha Mwembeni, Kata ya Mlimba, wilayani Kilombero.

Amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa kutokana na taarifa za raia wema na baada ya kuhojiwa na polisi amekiri kufanya mauaji hayo na ameweza kutoa ushirikiano kwa kuonesha sehemu alikoficha viungo hivyo.

Wakati huo huo jeshi hilo limefanikiwa kumkamata Jovina Mwakiyee (33) mkazi wa Kijiji cha Mang'ula A wilayani Kilombero, kwa tuhuma za kula njama na kumuua mume wake wa ndoa.

"Tukio hili limetokea Juni 1, mwaka huu majira ya usiku huko katika Kitongoji cha Gendeni, Kijiji cha Mang'ula A, wilayani Kilombero, ambapo mtuhumiwa huyo alikula njama zilizofanikisha kuuawa kwa mume wake huyo Christian Tungaraza (39) ambaye ni Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Signal," amesema kamanda Mkama.

Aidha, kamanda huyo amesema kuwa Mwalimu Tungaraza akiwa amelala na mtuhumiwa (mke wake), pamoja na watoto wao wawili, alivamiwa na kisha na kuuawa kwa kupigwa na kitu butu kichwani.

Amesema baada ya mauaji hayo Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi ili kuwapata watuhumiwa wengine ambao wadaiwa kushirikiana na mwanamke huyo.

Katika tukio jingine la mauaji, jeshi la polisi imefanikisha kuwakamatwa Hassan Mbwambo (31) ambaye ni mganga wa kienyeji na mkazi wa Same mkoani Kilimanjaro, John Matunda (20) dereva wa bodaboda mkazi wa Dumila wilayani Kilosa, Boniface Mwendi (31) Berega na Neema Mbwambo (32) wakazi wa Moshi vijijini, kwa tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara wa madini Elly Kimaro (53) mkazi wa jijini Arusha.

Kamanda Mkama amesema kuwa, tukio hilo la mauaji ya mfanyabiashara huyo lilitokea Mei 26 majira ya saa mbili usiku ambapo baada ya mauaji kufanyika, watuhumiwa hao walimnyang'anya sh. 15 milioni.

Imedaiwa kuwa kabla mauti haijamkuta, mfanyabiashara huyo alisafiri kutoka Arusha hadi Morogoro akiwa na Hassan Mbwambo ambaye ni mmoja wa watuhumiwa, na kisha kwenda Turiani kwa lengo la kufanya biashara za madini.

"Baada ya kufika eneo la Turiani mtuhumiwa kwa kushirikiana na mtuhumiwa mwenzake Samwel Matunda wakiwa na pikipiki walimteka hadi Kijiji cha Berega na kunyang'anyana kiasi hicho cha fedha na kumtaka mume wa marehemu kutuma kiasi kingine cha fedha sh. 5 milioni ili waweze kumuachia," amesema Kamanda Mkama.

Kamanda Mkama amesema kuwa baada ya kupatiwa kiasi hicho fedha watuhumiwa hao walimuua na kuutelekeza mwili wa mawanamke huyo katika shamba la mbaazi lililoko katika Kijiji cha Berega, hadi mwili huyo ulipoonwa na wasamalia wema.

Kufuatia matukio hayo ya mauaji hayo, Kamanda Mkama amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya wenza wao, kwa kuwa matukio mengi ya mauji huusishwa na mapenzi, japo amedai kuwa yapo mengine yanayohusishwa na imani za kishirikina, tamaa za kupata mali, fedha pamoja na migogoro ya kifamilia.