11 mbaroni tuhuma uharibifu miundombinu gesi, wizi madini

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 03:54 PM Oct 03 2024
Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro.
Picha:Mtandao
Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro.

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu 11 wakiwamo wanane wanaotuhuma kwa uharibifu wa miundombinu ya bomba la gesi la ORYX linalosafirisha nishati hiyo kutoka Bandari ya Dar es Salaam.

Wengine watatu  wanatuhumiwa kwa wizi wa madini aina ya Cooper Cathode (shaba) yaliyokuwa yakisafirishwa kutoka Congo kwenda Bandari ya Dar es Salaam.

Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, ameyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Aliwataja wanaoshikiliwa tuhuma za kuhujumu bomba la mafuta ni Twaha Salum (53) na wenzake saba.

“Watuhumiwa hawa wamehojiwa kwa kina na ushahidi umekusanywa na watafikishwa kwenye mamlaka zingine kwa hatua zaidi za kisheria,” alisema.

Kuhusu wanaotuhumiwa kuiba madini, Kamanda Muliro alisema, wanamshikilia Daudi Matola (50), ambaye ni dereva mkazi wa Kimara, wilayani Kinondoni, mkoani humo, na wenzake wawili kwa tuhuma zao.

Amesema tukio hilo lilitokea Agosti 7 mwaka huu, wakati dereva huyo na wenzake wawili wakiwa na gari T 882 DQK aina ya Benz na tela T 884 EEE mali ya Kampuni ya FAA Trucks, ambao baadaye walililitelekeza Dar es Salaam.

Kutokana na tukio hilo, Kamanda Muliro ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa na kuahidi kutokuwa na huruma kwa wahalifu na kuendela kuwashughulikia vikali kwa mujibu wa sheria.