WATU wanne wamefariki dunia na wengine 15 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wanasafiria la kampuni ya Kapricon kuacha njia na kupinduka.
Ajali hiyo ilitokea leo (Alhamisi) majira ya saa 7:30 usiku katika eneo la Mailikumi, wilayani Korogwe mkoani Tanga na kuhusisha basi lenye namba za usajili T 605 DJR.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi, Almachius Mchunguzi, amesema basi hilo lilikuwa linaendeshwa na Julius Mushi (43), Mkazi wa Arusha.
"Tumefuatilia na mpaka sasa waliopoteza maisha ni wanne ambapo wanaume watatu, mwanamke mmoja na wengine 15 wamejeruhiwa, majeruhi wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Wilaya (Magunga) lakini wengine wamepelekwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Bombo," amesema.
Kamanda Mchunguzi alitoa wito kwa madereva kuwa makini wakati wa kuendesha Kwa kufuatia sheria za barabarani ili kuzuia vifo na majeruhi ambayo vinaweza kudhibitiwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED