Riba mpya kukopa BoT hadi Disemba hii hapa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:08 PM Oct 03 2024
Gavana wa BoT  Emmanuel Tutuba.
Picha:Mtandao
Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba.

KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeeleza sababu za riba ya benki hiyo kuendelea kubaki asilimia sita (6) kwa robo mwaka inayoishia Disemba 2024.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolea leo (Alhamis) imeeleza sababu hizo kuwa ni matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kuwa chini ya lengo la asilimia tano.

Gavana wa BoT  Emmanuel Tutuba, alisema kamati inatarajia uchumi kuendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha, sambamba na kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi

“Uchumi wa dunia unatarajiwa kuendelea kukua sambamba na kuimarika kwa mazingira ya upatikanaji fedha. Kutokana na hali hii, Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia wanakadiria uchumi wa dunia kukua kwa asilimia 3.2 na asilimia 2.6, mtawalia, mwaka 2024,”amesema.

Amesema mwenendo huo unatarajiwa kuchagiza shughuli za uzalishaji nchini, na kwamba mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kupungua, ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi sambamba na kupungua kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, hususan mafuta na mbolea. 

Kwa mujibu wa Tutuba, kutokana na hali hiyo, benki kuu katika nchi nyingi zinatarajiwa kupunguza au kutokubadili riba zao za sera ya fedha. 

Vilevile, benki kuu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zinatarajiwa kufuata mwenendo huu wa kisera.