"Upatikanaji fedha za kigeni waimarika"

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:09 PM Oct 03 2024
Fedha za kigeni.
Picha:Mtandao
Fedha za kigeni.

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imesema kuwa upatikanaji wa fedha za kigeni uliimarika katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2024.

Aidha, imesema kuimarika huko kunakwenda sambamba na msimu wa shughuli za utalii na mauzo ya mazao ya kilimo na biashara nje ya nchi. 

Vile vile imesema kupanda kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia pia kulichangia ongezeko la mapato ya fedha za kigeni nchini. 

Hayo yamesemwa leo (Alhamisi) na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, katika taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania.

Amesema kutokana na mwenendo huu, kasi ya kuporomoka kwa thamani ya shilingi ilipungua hadi kufikia asilimia 10.1 kwa mwaka unaoishia Septemba 2024, kutoka asilimia 12.5 kwa mwaka ulioshia Juni 2024. 

“Akiba ya fedha za kigeni iliongezeka kufikia dola za Marekani milioni 5,413.6 mwishoni mwa Septemba 2024 kutoka dola za Marekani milioni 5,345.5 mnamo Juni 2024,”amesema.

Tutuba amesema kuwa akiba hiyo inatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa zaidi ya miezi 4, ambayo inaendana na lengo la nchi.

“Upatikanaji wa fedha za kigeni unatarajiwa kuendelea kuimarika, kutokana na ongezeko la bei ya dhahabu kwenye soko la dunia, shughuli za utalii na mauzo ya bidhaa asilia kama korosho, tumbaku, kahawa na pamba,”amesema.

Aidha, amesema mauzo ya mazao ya chakula hususan mahindi na mchele kwenda nchi jirani, pia yanatarajiwa kuongeza mapato ya fedha za kigeni. 

Gavana huyo amesema kuwa kupungua kwa uagizaji wa mbolea na kupungua kwa bei za bidhaa za mafuta ya nishati kunatarajiwa kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni.

Vilevile, matakwa ya kisheria kuhusu kunukuu na kufanya malipo ya ndani kwa shilingi ya Tanzania yanatarajiwa kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni nchini na kuongeza ufanisi wa sera ya fedha.