Adaiwa kuua mke kisha kujiua, aacha ujumbe wa majuto

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 10:59 AM Oct 03 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilibroad Mutafungwa
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilibroad Mutafungwa

DERVINUS Nkabatina (46), Mfanyabiashara na Mkazi wa Nyamhongolo wilayani Ilemela mkoani Mwanza anadaiwa kumuua mke wake Rausa Mohamed (36), kwa kumsukuma na kuanguka kwenye sakafu kisha kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni.

Nkabatina, anadiwa siku mbili baada ya kutekeleza tukio hilo alipotelea kusikojulikana kisha baadae kuonekana kwenye baa ijulikanayo wa jina la Ndama alikoenda kunywa dawa kwa kutumia kilevi aina ya Konyagi kwa lengo la kujiua na ukutwa na ujumbe ulionesha kujutia tukio alilolitenda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mapema jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilibroad Mutafungwa ilisema walipokea taarifa za mauaji ya Mwanamke huyo Septemba, 28 mwaka huu majira ya saa 4:45 usiku kutoka kwa majirani zao.

Kamanda Mutafungwa uchunguzi wa awali unaonesha kulikuwa na gogoro wa ndoa, mke akimtuhumu mume wake kutoka nje ya ndoa. Kamanda aliongeza kuwa baada ya tukio hilo majirani walifika kwa ajili ya kutoa msaada na taarifa zilifika kwa Jeshi la Polisi, hatimaye mwanamke huyo alipelekwa katika kituo cha afya Igoma.

Alisema wakati madaktari wanajaribu kuokoa maisha yake alifariki dunia. Mtuhumiwa baada ya tukio hilo alikimbia kusikojulikana na jitihada za kumtafuta zilianza mara moja. Marehemu Rausa Mohamed ameacha mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja.

Kamanda Mutafungwa alisema wakati waliendelea na msako  Septemba, 30, 2024 majira ya saa Saba mchana walipata taarifa kwamba ameonekana akinywa pombe katika baa ijulikanayo kwa jina la Ndama.

"Jeshi la Polisi lilifika katika bar hiyo na kumkuta mtuhumiwa akiwa amedhoofika, tulipata taarifa kutoka kwa wahudumu wa baa hiyo kuwa Nkabatina alifika akiwa ameshika bahasha yenye rangi ya khaki na kuagiza pombe aina ya konyagi chupa yenye ujazo wa miligram 750, kisha alimeza vidonge ambavyo idadi yake haikuweza kufahamika kwa kutumia pombe aliyokuwa ameagiza ndipo hali yake ilianza kubadilika ikawalazimu watoe taarifa kwa Jeshi la polisi," alisema DCP Mutafungwa. 

Alisema baada ya upekuzi alikutwa na  mabaki ya dawa aina ya Metronidazole na kiasi cha pombe aina ya konyagi kwenye chupa, pia alikutwa na karatasi yenye ujumbe usemao “Shetani ameanza kuniita ewe Mwenyezi Mungu roho yangu naikabidhi mikononi mwako”.

Kadhalika Karatasi hiyo pia ilikuwa na maandishi mengine yanayoonesha majuto ya kitendo cha kumuua mke wake na kuwa amefanya maamuzi ya kujiua na angependa mwili wake usipelekwe kwao Karagwe bali uzikwe Mwanza. 

Alisema Nkabatina alikimbizwa katika hospital ya Sekeo-Toure hata hivyo alifariki dunia wakati matibabu yakiendelea.

"Chanzo cha matukio haya ni wivu wa kimapenzi, kwani inadaiwa mwanamke alikuwa akimtuhumu mume wake kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanawake wengine na mume wake aliamua kujiua ili kukwepa mkono wa sheria baada ya kufanya maamuzi yasiyo faa kwa kumshambulia mke wake na hatimae kumuua," alisema DCP Mutafungwa