Myovela: Kuna vitu vinapaswa virekebishwe TRA

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 06:22 PM Oct 03 2024
MSHAURI wa masuala ya kodi kutoka Kampuni ya OASIS, Stambuli Myovela.
Picha: Maulid Mmbaga
MSHAURI wa masuala ya kodi kutoka Kampuni ya OASIS, Stambuli Myovela.

MSHAURI wa masuala ya kodi kutoka Kampuni ya OASIS, Stambuli Myovela amesema kutokana na utafiti waliofanya wamegundua kwamba kuna vitu ambavyo vikiboreshwa zitasaidia biashara kukuwa na kupunguza migomo na shida zinazoendelea katika jumuiya za wafanyabiashara.

Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam wakati wa Kongamano la Kodi lililoandaliwa na OASIS, mshauri huyo amesema kongamano hilo lina lengo la kuwaunganisha wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), pamoja na kuhakikisha kwamba wanasaidia biashara kukuwa.
 
Amesema sehemu ambayo wanapata changamoto sana ni katika uingizaji wa mizigo kutoka nchi nyingine, akieleza kuwa upande huo umekuwa changamoto sana sio kwa mfanyabiashara peke yake bali hata kwa wakaguzi wa TRA wamapokenda kukagua.
 
“Lakini pia ukisoma vitabu vya mahesabu vya watu wa kariakoo (wafanyabiashara) au vya watu wanaoingiza bidhaa ni changamoto hakuna nyaraka na vitabu vya kutosha, na imefikia kuna wakati wanaoingiza bidhaa wanashindwa kupata haki zao stahiki pale matatizo yanapotokea kama insurance clam,” amesema Myovela.
 
Ameongeza kuwa wanapokosa nyaraka za kila aliyeingiza mzigo hata chanzo kwenye kodi za ndani wanakuwa wanalipa kodi kubwa kwasababu wanaonekana wanapata faida kubwa kwa kukosa vithibitisho vinavyoeleweka vya kibiashara.
 
Pia ameshauri wafanyabishara kujitahidi kufwata hatua zote za kusheria wakati wanapoingiza bidhaa zao kwenye mifumo ya forodha iwe sahihi.
 
Wakati huo huo, ameeleza kuwa sheria ambazo zipo zinatoza viwango vikubwa vya kodi wakati wa uingizaji wa bidhaa, akishauri mamlaka kwamba inaruhusiwa kisheria kuishauri serikali kutokutumia sheria za Afrika Mashariki ambazo zinatoza ‘import intra’ ya asilimia 25 na 18.
 
Amesema wanaweza kuomba kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokutumia viwango hivyo vya Afrika Mashariki kwasababu ndivyo viwango ambavyo vinasukuma sana ukwekaji wa kodi, na kwamba wanaweza kutumia viwango hivyo katika bidhaa ambazo ni muhimu.
 
“Ni muda mzuri wa kujielekeza sana katika kuanzisha viwanda vya ndani hasa katika sekta muhimu zilizopewa vivutio vikubwa vya kodi, hiyo itatupunguzia kulipa kodi nyingi bandarini na kutuma fedha nyingi nje ambazo zitasaidia katika kukuza uchumi wa nchi yetu,” ameshauri Myovela.
 
Kamishna Idara ya Walipakodi Wakubwa TRA, Michael Muhoja, amesema kitu ambacho wanakitamani ni kuwa na uwanja sawa wa kila mmoja kufanya shughuli zake kwa usawa bila yoyote kuhisi kwamba hatendewi haki au anaonewa.
 
“Kama ni watu ambao tunalitakia mema taifa hili tufwate sheria na utaratibu uliopo, kama unafanya ‘importation’ agiza mzigo wako upite katika chaneli ambazo ziko sawa na mwisho wa siku kila mmoja aweze kuhakikisha kwamba amefanya biashara katika uwanja ambao uko sawa sawa.
 
“Tukifanya biashara kila mtu kivyake hiyo ndo changamoto kubwa, tunataka kwamba tuwe na uwanja wa kuchezea ambao uko ‘flat’ na fujo nyingi ambazo tunaziona zinatokana na hiyo ‘inequality’ kuna wanaolipa na wasiolipa kodi, hawatendi haki katika taifa hili, ni wito wa TRA kuwahimiza kwamba kila mtu alipe kodi,” amesisitiza Muhoja.