WAZIRI Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu, ameapa kulipiza kisasi dhidi ya Iran kwa kile alichodai kuwa mashambulizi yaliyofanyika ni uchokozi mkubwa kwa taifa hilo.
Aidha, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) limefanya kikao cha dharura usiku wa kuamkia Oktoba 2,2024 kujadili mzozo unaozidi kutanuka wa Mashariki ya Kati.
Pia Iran nayo imejibu kupitia Rais Masoud Pezeshkian ikitishia kwamba itajibu vikali zaidi iwapo Israel itathubutu kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi.
Balozi wa Iran kwa UN aliliambia baraza hilo kwamba madhumuni ya nchi yake kurusha dazeni ya makombora nchini Israel ni kwa ajili ya kuzuia taifa hilo kutoendelea na mashambulizi yake.
Usiku wa kuamkia Jumatano, Iran ilivurumusha makombora ya masafa marefu yapatayo 180 kuelekea Israel ikisema ilikuwa ikiyalenga maeneo na miundombinu ya kijeshi.
Israel ilisema asilimia kubwa ya makombora hayo yalinaswa na kuharibiwa na mfumo wa ulinzi wa anga kwa kusaidiwa na washirika wake kama Marekani, Uingereza na Ufaransa.
Lakini Tehran ilisisitiza kuwa makombora yake mengi yalilenga shabaha zao huku Mkuu wa Majeshi wa Iran Mohammad Bagheri, akiionya Israel kuwa isipojizuia, operesheni hiyo ya juzi usiku inaweza kujirudia.
Wakati huo huo, Balozi wa Israel katika Umoja huo wa Mataifa, Danny Danon alisema hatua hiyo ya Iran kuishambulia Israel ni kitendo kikubwa cha uchokozi na iwapo haitozuiliwa basi wimbi jengine la makombora halitoilenga tu Israel bali mataifa mengine pia.
Rais wa Marekani, Joe Biden alisema kuwa hatoiunga mkono Israel iwapo itashambulia miundombinu ya zana za nyuklia za Iran.
HALI YA HATARI
Wakati hayo yakiendelea, ilielezwa kuwa Israel ambayo inapambana na wanamgambo katika ngome mbili, ikiwamo kundi la Hezbollah katika uvamizi wake wa ardhini nchini Lebanon pamoja na wanamgambo wa Hamas huko Gaza, imefanya mashambulizi yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa juzi.
Ilielezwa kuwa Naibu Kansela wa Ujerumani Robert Habeck, alisema hali ya Mashariki ya Kati ni hatari, akishauri kuwa kuna haja ya Ujerumani kushikamana na Israel huku akitoa wito wa diplomasia kutumika katika usitishwaji mapigano.
Jeshi la Israel lilitoa amri jana ya kuwataka watu waondoke katika maeneo kadhaa ya kusini mwa Beirut huko Lebanon, yaliyo na idadi kubwa ya watu, ikisema itayashambulia maeneo ya wanamgambo wa Hezbollah katika eneo hilo.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa Israel tayari imefanya mashambulizi katikati mwa mji huo mkuu wa Lebanon na kusababisha vifo vya watu sita. Huku Wizara ya Afya ya Lebanon ikisema watu wengine saba wamejeruhiwa katika shambulizi hilo la usiku wa kuamkia jana.
Vile vile, ilielezwa kuwa Jeshi la Israel kwa upande wake limepata pigo pia kwani limethibitisha kwamba wanajeshi nane wameuawa, huku saba wakijeruhiwa vibaya kusini mwa Lebanon kutokana na mashambulizi ya wanamgambo wa Hezbollah.
Ilielezwa kuwa, vifo vya wanajeshi hao ndiyo mauaji ya kwanza ya wanajeshi wa Israel tangu ilipoanzisha mashambulizi ya ardhini huko Lebanon mapema wiki hii.
Wakati hayo yakiendelea, ilielezwa kuwa maelfu ya raia wa Lebanon wanaendelea kumiminika nchini Syria wakiyakimbia mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon.
Kikosi cha waandishi wa habari wa shirika la habari la Associated Press, kilisema kimeshuhudia mamia ya watu wakikusanyika katika kivuko cha mpakani cha Jousieh, ambacho ni mojawapo ya njia za kuingia Syria.
APE/AFP/DW
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED