TATIZO la uchafuzi wa mazingira ya bahari limekuwa changamoto kubwa inayohitaji kushughulikiwa haraka, fukwe nyingi, hususan za jijini Dar es Salaam, zimekumbwa na ongezeko la taka, hasa taka za chupa za plastiki na vifaa vya kufungashia, pamoja na taka hatarishi kama sindano na taulo za kike.
Hali hiyo imekuwa ikiathiri mazingira ya bahari, viumbehai, na matumizi ya fukwe kama sehemu za utalii, kutokana na tatizo hilo, juhudi mbalimbali zimeanzishwa ili kupambana na uchafuzi huo, huku vijana wakiwa mstari wa mbele katika kutafuta suluhisho.
Vijana wamepewa nafasi maalumu kushiriki katika juhudi za uhifadhi wa bahari kupitia mafunzo yanayolenga kuwawezesha kuwa mabingwa wa kuhifadhi fukwe na mazingira ya bahari.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea vijana uwezo wa kutambua aina za taka, kuzianisha, na kuzichakata sambamba na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira ya bahari.
Vijana wanafundishwa pia kufanya tathmini ya taka na kuchukua hatua za kuzuia taka hizo zisitoke kwenye mito na mifereji hadi kufika baharini.
Sara Pima, Mkurugenzi wa Taasisi ya Human Development and Environment Foundation (HUDEFO), ameeleza kuwa taasisi hiyo imeendesha mafunzo kwa vijana wapatao 50 kwa njia ya mtandao na vitendo.
Amesema lengo ni kuwawezesha vijana hao kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira, hususan katika maeneo ya fukwe, yanawawezesha pia kuangalia fursa zinazopatikana kutokana na shughuli za uhifadhi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kuzifanyia uchakataji taka zinazokusanywa fukweni, na hivyo kuwasaidia vijana kupata ajira.
Vikundi vya vijana, kama Ocean Champs na Ocean Bee’s, vilivyoundwa na vijana walionufaika na mafunzo ya HUDEFO, vimekuwa vikiendesha shughuli mbalimbali za usafi wa fukwe, huku wakitumia utaalamu walioupata kufanya tathmini ya taka hizo.
“Ujuzi huu unawafanya vijana wawe wabobezi katika kutekeleza majukumu yao ya uhifadhi wa fukwe kwa ufanisi zaidi kuliko makampuni mengi yanayojihusisha na usafi wa fukwe bila kuwa na utaalamu wa kutosha,” amesema Pima.
Rehema Ally, mmoja wa vijana walionufaika na mafunzo hayo, amesema tatizo la uchafuzi wa bahari linachangiwa na utupaji hovyo wa taka kwenye mito, mifereji, na zinaishia baharini.
Amesema matokeo ya vitendo hivyo ni kuharibu ikolojia ya bahari pamoja na viumbehai wanaoishi ndani yake.
Amina Uledi, Mwenyekiti wa kikundi cha Ocean Champs, amesema kuwa kutokuchukua hatua za haraka katika kukabiliana na tatizo hili kutaweka viumbehai wa baharini kwenye hatari ya kupotea kabisa.
Hata hivyo Pima imeiomba serikali, pamoja na wadau mbalimbali, kushirikiana nao kuendeleza jitihada hizo za vijana, amesisitiza umuhimu wa serikali kuweka sheria kali za kudhibiti utupaji wa taka za plastiki na kulinda bahari kwa maslahi ya sasa na ya baadaye.
Simon Kimaro, mfanyakazi wa HUDEFO, ameongeza kuwa uchafuzi wa bahari pia unachangiwa na uvuvi haramu unaotumia kemikali, ambao unaharibu mazingira ya baharini na kuzorotesha maisha ya viumbehai.
Hadi sasa vikundi hivyo vimefanya usafi kwenye fukwe za Maga na Rainbow zinazopatikana jijini Dar es Salaam.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED