Mchungaji kuchunguzwa madai kuendesha maombi chonganishi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:42 AM Oct 03 2024
Mchungaji kuchunguzwa madai  kuendesha maombi chonganishi
Picha:Mtandao
Mchungaji kuchunguzwa madai kuendesha maombi chonganishi

SERIKALI mkoani Simiyu imeanza uchunguzi dhidi ya huduma zinazotolewa na Mchungaji wa Kanisa la International Evangelical Assembles of God Tanzania (IEAGT) kwa madai ya kufanya maombezi chonganishi.

Uchunguzi huo umeanza kutokana na agizo lililotolewa juzi na Mkuu wa Mkoa, Kenani Kihongosi, kwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Shishiyu katika ziara yake ya kikazi iliyolenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Kigonhosi alisema maombezi yanayofanywa katika kanisa hilo ni chonganishi kutokana na watu kutajwa majina wakati wa maombi kuwa ni wachawi kwa madai kuwa mapepo yamepanda.

“Mkuu wa wilaya hili suala liko chini yako na fuatilia uhalali wa kanisa hili. Haiwezekani  mchungaji aendeshe ibada zinazotaja majina ya watu na kuwatuhumu kuwa ni wachawi kisa mapepo yamepanda. Hizi  ni ramli chonganishi kama zingine,” aliagiza.

Kihongosi alimtaka mchungaji huyo kuhakikisha mapepo hayo hayataji tena majina ya wakazi wa eneo hilo kwa kuwa ibada hiyo inaleta taharuki kwa wananchi na kuwafanya waishi maisha ya hofu.

“Wewe kama ni mtaalamu wa kuzungumza na mapepo, sasa yaambie hayo mapepo yaache kutaja majina ya watu na kuwatuhumu kuwa ni wachawi na unajua serikali ina uwezo wa kufungia kanisa lolote linalohatarisha usalama wa wananchi,” alisema Kihongosi.

Akitoa utetezi katika mkutano huo, Mchungaji wa Kanisa hilo, Joseph Jackson, alisema hajamtuhumu mtu yeyote kuwa ni mchawi isipokuwa ni waumini wanaofika kanisani hapo kufanyiwa maombi na kuwa mapepo yakipanda, wanaanza kutaja majina ya wachawi hao.

“Mkuu wa Mkoa mimi sijawahi kumtaja mtu yeyote kuwa ni mchawi. Wanaonituhumu  waseme vizuri. Mimi  natoa huduma ya kuombea watu walio na mapepo nikiyauliza yametoka wapi ndipo huwa yanawataja,” alisema.

Awali, akitoa malalamiko kwa mkuu huyo wa mkoa,  mmoja wa waathirika wa maombezi ya mchungaji huyo, Pili Kidesela, mkazi wa kata ya Shishiyu, alisema  mchungaji huyo amekuwa kero kwa wakazi wa eneo hilo kwa kuendesha ibada zinazowatuhumu wakazi hao kuwa wachawi.

“Nimetuhumiwa kuwa ni mchawi na si mimi peke yangu bali wakazi wengine hapa Shishiyu wametuhumiwa uchawi.  Hii hali inatufanya tuishi kwa hofu katika eneo letu kutokana na huduma yake huyu mchungaji,” alisema  Kidesela.

Mkazi mwingine, Lucia Marko, alisema katika maombezi ya mchungazi huyo amewahi kutajwa kuwa mmoja wa wachawi wanaowaloga waumini wa kanisa hilo.

“Mimi nilishatuhumiwa kuwa huwa naenda kanisani hapo kuwaloga waumini wa kanisa hilo. Nilituhumiwa  hivyo baada ya muumini wa kanisa hilo kupandisha mapepo na kunitaja kuwa aliniona,” alisema.

Naye Marko Mashauri alisema mchungaji huyo amekuwa akiendesha ibada hizo chonganishi kwa kutaja majina ya wanawake kijijini hapo na kuwatuhumu kuwa  wachawi.

Nipashe ilimtafuta mtendaji wa kata hiyo ili kujua kama amewahi kupokea malalamiko ya namna hiyo na alikiri kuyapokea na kuwa alishawahi kumwita na kumtaka aachane na mafundisho hayo lakini hakuwa tayari kufanya hivyo.

Alisema baada ya hapo, ilibidi atoe taarifa kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Aswege Kaminyoge, aliyeahidi kulifanyia kazi ili kudhibiti taharuki iliyozuka kwa wananchi wake.

Naye Kaminyoge alisema licha ya uchunguzi juu ya maombezi ya mchungaji huyo, amewahi kukutana naye awali na kumzuia masuala hayo lakini hakuwa tayari kutii agizo hilo.