MATUMIZI sahihi ya kiwango cha dawa ya meno kwenye mswaki, kabla ya kuswaki kinywa ni chanzo cha kuyakinga dhidi ya kuoza na kutoboka, imeelezwa.
Aidha, ubora wa dawa za meno zenye madini ya floridi, umeelezwa kuongeza ulinzi wa meno kwa kuyakinga dhidi ya kuoza.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kinywa na Meno katika Wizara ya Afya, Dk. Baraka Nzobo, aliyasema hayo, hivi karibuni wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii.
Alisema ili kujikinga na meno dhidi ya kuoza, inashauriwa kupiga mswaki meno mara mbili kwa siku (asubuhi na usiku kabla ya kulala) kwa kutumia dawa yenye madini ya floridi iliyo na ubora.
“Kuanzia jino la kwanza linapoanza kuota na hadi miaka miwili, weka dawa ya meno kwa ukubwa wa punje ya mchele (900-1000 ppmF- Dawa ya meno maalumu kwa watoto).
“Kwa wenye miaka mitatu hadi mitano, weka dawa ya meno kwa ukubwa wa punje ya harage 9900-1000 ppmF-Dawa ya meno maalumu kwa watoto). Miaka sita mpaka umri wa mtu mzima, weka dawa ya meno ijae eneo lote la brashi ya kwenye mswaki (1400-1500 ppmF-dawa ya meno ya watu wazima),” alisema.
Dk. Nzobo alisisitiza kwa kutoa wito kwa wananchi kwamba matumizi sahihi ya dawa ya meno na yenye kiwango cha ubora wa madini ya floridi na ujazo wa kila siku huundoa athari hasi kwa kinywa.
Alisema kiwango cha wagonjwa wanaopatiwa matibabu ya kinywa na meno nchini inakua huku akibainisha kuwa kuanzia Julai, mwaka jana, hadi Juni, mwaka huu, watu 535,324 waliohudhuria kwenye vituo vya kutolea matibabu nchini, walibainika kuoza meno.
Kati yao, alisema wagonjwa 219,482 sawa na asilimia 41, walifanyiwa matibabu ya kuziba jino (kutibu jino) kwa kuziba kwa dawa ya kudumu; kuziba kwa dawa ya muda na kutibu mzizi wa jino (root canal treatment).
Alisema lengo kuu la serikali kupitia Wizara ya Afya ni kuhakikisha inatibu meno ya watu kwa asilimia 60 na si kuyang’oa.
“Kabla ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali, miaka ya nyuma tulikuwa tunaziba kwa asilimia mbili na kung’oa watu meno kwa asilimia 98. Kwa sasa mambo yamebadilika na yatazidi kuwa bora zaidi mpaka lengo la kuziba kwa asilimia 60 litakapofikiwa ndani ya muda mfupi.
“Hospitali za rufani za mikoa zinazoziba meno watu wengi kuliko kung'oa ni 23 nchini ikiwamo Hospitali ya Rufani ya Kanda Mbeya (MZRH). Zingine zenye hadhi ya rufani kimkoa ni Mawenzi, Mount Meru Njombe, Simiyu, Mwalimu Nyerere Memorial, Temeke, Songwe, Singida, Manyara, Iringa, Geita na Bukoba.
“Pia zimo Amana, Morogoro, Dodoma, Sekotoure, Sumbawanga, Tanga, Sokoine, Shinyanga, Maweni na Shinyanga,” alisema.
Dk. Nzobo alizitaja pia hospitali 38 za wilaya nchini zinazoziba meno (kuyatibu) kwa wingi kuliko kuyang'oa ni Makambako, Arusha, Bagamoyo, Bariadi, Bukombe, Chato, Frelimo na Geita.
Zingine ni Hai, Handeni, Igunga, Ikungi, Kalambo, Karagwe, Kigamboni, Kiomboi, Kondoa, Korogwe, Kyela, Ulanga, Mbarali, Meru, Misungwi-Iteja, Monduli, Mtowisa, Muheza, Ngorongoro, Nsimbo, Nzega, Rombo, Rorya na Siha.
“Pia hospitali za Singida, Tanganyika, Tukuyu, Uvinza, Wanging'ombe na Vwawa inatibu maradhi hayo. Tanzania bila vibogoyo au watu wenye mapengo inawezekana,” alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED