SHIRIKA la Viwango Zanzibar (ZBS), limesema wakala asiye na namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN), anayefanyakazi ya kutoa mizigo katika bandari visiwani humo, hatohudumiwa.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Yusuph Majid Nassoro, ameyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa kusaini mkataba wa ushirikiano katika ukusanyaji wa kodi za forodha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Amesema ZBS na TRA, zitashirikiana kwa kupeana taarifa zitakazorahisisha ufanyaji wa biashara na hivyo kuongeza mapato na tozo za serikali.
Amesema moja ya taarifa ni za wafanyabiashara wanaotumia bandari za Zanzibar, ambao ili ZBS ihakiki mizigo yao, ni lazima wawe na TIN.
“Na hili litafanyika kwa urahisi sana kwa sababu mifumo yetu inasomana na TRA, kwa hiyo hakutakuwa na haja ya mfanyabiashara kuja ofisini kwetu, anaweza kufanya kila kitu kwenye mtandao na kutuma kwetu, sisi tukashughulikia,” amesema.
Naye, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema makubaliano hayo yanalenga kuongeza uwazi na kurahisisha ufanyaji wa biashara visiwani humo.
“Tunataka kuongeza usalama wa mizigo inayoingia, kuongeza kasi ya uondoshaji (clearing) na kupunguza muda na vikwazo. Makubaliano haya ni kurahisisha jukumu la TRA la kukusanya kodi za forodha nchini yaani Bara na Zanzibar,” amesema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED