JESHI la Polisi mkoani Dodoma linawashikilia watu watano wakiwamo madereva wawili kwa tuhuma za kusafirisha gunia 15 za bangi.
Gunia hizo zilikamatwa juzi ndani ya basi la kampuni ya New Best line eneo la Stendi ya Mabasi Nanenane lililopo mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geoge Katabazi alisema basi hilo lenye namba za usajili T 882 EBS lilikamatwa katika msako unaoendelea kukamata wahalifu wa matukio mbalimbali.
Kamanda Katabazi alisema basi hilo lilikuwa likitokea Tarime kuelekea Dar es Salaam, baada ya kufika Stendi ya Nanenane mkoani hapa, askari waliokuwa doria wakifanya ukaguzi walilitilia mashaka na baada ya kupekua walibaini uwepo wa gunia hizo za bangi ndani ya buti.
Alisema watuhumiwa hao wamefikishwa kituo cha polisi pamoja na basi hilo wakati uchunguzi ukiendelea kutokana na tuhuma za tukio hilo ambalo huleta athari kubwa kwa jamii.
"Matumizi ya dawa za kulevya aina bangi zina madhara makubwa sana, ndizo husababisha masuala ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji,"alisema Kamanda Katabazi.
Alisema watu wanapotumia bangi huchangia kuongezeka kwa uhalifu kwa sababu wanapozivuta huwasababishia kufikiria kufanya uhalifu.
Kadhalika, alitoa rai kwa madereva wa vyombo vya moto kuwa makini na mizigo inayosafarishwa ili kujiweka salama na kazi wanazozifanya.
Kamanda Katabazi alisema jeshi hilo linaendelea na msako katika maeneo mbalimbali mkoani hapa, huku likisisitiza wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kusaidia kukamata uhalifu unaofanywa.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi limeendelea kusisitiza jamii kusherehekea Sikukuu ya Christmas na Mwaka mpya kwa utulivu bila kufanya vurugu yoyote katika maeneo mbalimbali mkoani hapa.
Alisema jeshi hilo linaendelea na doria katika maeneo tofauti jijini Dodoma ili kuwabaini wahalifu waliopanga kufanya matukio.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED