Wakulima waonywa kuficha mifugo kupatiwa chanjo

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 09:04 AM Dec 26 2024
Wakulima waonywa kuficha mifugo kupatiwa chanjo
Picha: Mtandao
Wakulima waonywa kuficha mifugo kupatiwa chanjo

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Abdul Mhinte amewaagiza viongozi wa vyama vya wafugaji kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa wakati wa chanjo ya mifugo itakayoanza Januari mwakani ili kuhakikisha wafugaji hawafichi mifugo.

Akizungumza juzi wakati akifunga kikao kazi cha  uhamasishaji kampeni ya chanjo kitaifa kilichokuwa kinafanyika jijini Dodoma, Mhinte alisema wafugaji wahakikishe wanatii Sheria ya Magonjwa ya Wanyama ya Mwaka 2003 na Kanuni za Chanjo na Uchanjaji za Mwaka 2020.

"Unakuta mfugaji ana ng'ombe 500 halafu anachanja 100, wengine anawaficha porini. Baadaye zoezi letu linaonekana lina shida, niwaombe viongozi wa vyama vya wafugaji na wafugaji tushirikiane, msifiche mifugo wakati wa uchanjaji," alisema.

Mhinte pia aliwahimiza wafugaji kuendeleza maeneo ya malisho ya mifugo yatakayosaidia kuondoa migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. 

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Dk. Benezeth Lutege alisema chanjo ya mifugo itakayotolewa awamu hii inazalishwa na Serikali ya Tanzania na imethibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA), hivyo wafugaji wathamini chanjo zinazozalishwa nchini.

"Kampeni yetu itatumia chanjo inayozalishwa na Viwanda vyetu vya ndani, ni chanjo salama na imethibitishwa na  TMDA. Pia imepata kibali cha maabara ya Kanda ya Afrika  na tumekuwa tukisafirisha hata nje ya nchi," alisema.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho, Gabriel Bura, alisema chanjo ya mifugo inapaswa kwenda sambamba na uzalishaji malisho ili mifugo inapochanjwa iwe imepata chakula kuwezesha chanjo hiyo kufanya kazi.

Makamu  Mwenyekiti wa Chama cha Ufugaji Tija (CHAMAUTA), Ester Moreto, alisema elimu inahitajika kuongeza uelewa kwa wafugaji ili kutokomeza magonjwa ya mifugo na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo yanayozalishwa nchini.

"Mimi nina miaka minne ninachanja ng’ombe wangu na hawajawahi kuwa na shida yoyote. Niwaombe wafugaji wenzangu wasifiche mifugo, wachanje wote. Pia serikali itoe elimu na hamasa kwa wafugaji kote nchini," alisema.

Katika awamu ya kwanza ya mpango huo wa chanjo, serikali kupitia wataalamu wa Sekta ya Mifugo na Mamlaka za Serikali za Mitaa inatarajia kuchanja ng’ombe 19,097,223  dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu ya ngo’mbe (CBPP), mbuzi na kondoo 20,900,000 dhidi ya ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo (PPR).

Kuku wa asili 40,000,000 watachanjwa dhidi ya ugonjwa wa mdondo wa kuku (ND) ambapo lengo la serikali ni kutoa chanjo kwa mifugo angalau asilimia 70 ya idadi ya mifugo husika kwa miaka mitano mfululizo.