WAKULIMA wa Tumbaku wa Chama cha Msingi cha Ushirika Lualaje (Lualaje AMCOS) katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, wametakiwa kulipa madeni yao kwa wakati, ili kuepuka mali zao kushikiliwa na kupigwa mnada.
Mwenyekiti wa chama hicho, Alberto Kacheza alitoa wito huo juzi kwenye mkutano mkuu wa mwaka uliolenga kupitia taarifa ya mapato na matumizi pamoja na kufanya tathimini ya uzalishaji wa tumbaku na kupanga mikakati ya kuongeza tija.
Kacheza alisema wapo baadhi ya wakulima kwa makusudi wamekuwa wakilimbikiza madeni ya mikopo ya pembejeo hali inayosababisha kupata hati zenye mashaka.
“Tutaanza kuwachukulia hatua wakulima wasiorejesha mikopo, kupitia mkutano huu wakulima wamependekeza walio na madeni na kushidwa kurejesha mali zao kama mashamba yapigwe mnada kulingana na deni husika,” alisema Kacheza.
Alisema msimu huu wamejiwekea malengo ya kuongeza uzalishaji kutoka kilo milioni 1.3 mpaka 1.5 kulingana na hali ya hewa pamoja na mahitaji ya soko la zao hilo.
Alisema msimu uliopita wa kilimo kulikuwa na tatizo katika uzalishaji lililotokana na mabadiliko ya tabianchi na hivyo kutofikia malengo ya uzalishaji waliojiwekea.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Wilaya ya Chunya (CHUTCU), Isaya Hussen aliutaka uongozi wa ushirika huo kuwa na mipango madhubuti ya ukusanyaji wa madeni ili kuepuka baadhi ya wanachama kulimbikiza.
Alishauri chama hicho kuwa na mfuko wa pembejeo wa ushirika ambao utakuwa msaada kwa wakulima na kuacha kusubiri ruzuku kutoka serikalini akidai kuwa wakati mwingine huwa inachelewesha.
Ofisa Tarafa wa Kipembawe, Kassim Salum alisema serikali imetoa maelekezo kwa viongozi wa Amcos kuanza kuwachukulia hatua wakulima walioshindwa kulipa madeni ikiwemo kutaifisha mali zao ili kufidia madeni hayo.
Alisema wapo wakulima kwa makusudi wanakwepa kulipa madeni na kutorosha maroba ya tumbaku kuuza maeneo mengine, hivyo lazima wawajibishwe kwa mali na mashamba yao kupigwa mnada kwa mujibu wa kanuni na sheria zitakavyoelekeza.
Alisema katika kuhakikisha kilimo cha tumbaku kinafanya vizuri wamechukua sampuli za udongo 500 kwa ajili ya kufanya utafiti na aina ya mazao yatakayozalishwa ili kuongeza tija ya uzalishaji wa zao hilo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED