Wakulima wa korosho Ndanda wafunga barabara kushinikiza kulipwa fedha zao

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:07 PM Nov 06 2024
Wakulima wa korosho Ndanda wafunga barabara kushinikiza kulipwa fedha zao
Picha: Hamis Nasri
Wakulima wa korosho Ndanda wafunga barabara kushinikiza kulipwa fedha zao

Wakulima wa zao la korosho katika Kata ya Ndanda, wilayani Masasi, Mkoa wa Mtwara, wamefunga barabara kuu ya Masasi kuelekea Lindi na Mtwara wakishinikiza malipo ya korosho zao.

 Tangu kuanza kwa msimu na minada ya kwanza hadi wa tatu, bado hawajalipwa malipo yao, hali ambayo imezua hasira na kusababisha hatua hiyo ya kufunga barabara kwa magogo na mawe leo asubuhi.

Kutokana na kitendo hicho, magari yaliyokuwa yakisafiri kutoka Masasi kwenda Lindi na Mtwara yalikwama kwa takriban saa tatu. Wakulima hao wameeleza kuwa wanaomba malipo ya korosho zao yafanyike haraka, wakisema kuwa kucheleweshwa kwa malipo hayo kunatokana na Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi-Mtwara na Nanyumbu (MAMCU) kutochukua hatua stahiki.

Mmoja wa wakulima, Juma Athumani, amesema wamechukua hatua hiyo kali ili kushinikiza serikali na mamlaka zinazohusika kuhakikisha malipo yanatolewa. "Hatutaondoka hapa mpaka tupate fedha zetu," amesema Athumani kwa msisitizo.

Ayubu Michael, mkulima mwingine kutoka Ndanda, amesema kuwa wapo wakulima ambao hawajalipwa tangu mnada wa kwanza na hawajui sababu ya kuchelewa kwa malipo yao. Wakati huohuo, Asha Salumu amelalamikia kutolipwa licha ya kuuza mazao yao kwa wakati.

Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Lauter Kanoni, amewasili eneo hilo na kuwataka wakulima kuwa na subira, akieleza kuwa serikali inafanyia kazi suala hilo. Amesema tayari baadhi ya wakulima wameshaanza kulipwa na serikali imekutana na viongozi wa ushirika na benki ili kushughulikia changamoto hiyo.