Wadau wa kilimo waitwa kutoa elimu uzalishaji mbegu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:45 PM Nov 05 2024
Wakulima wa mpunga wakipewa mafunzo ya uzalishaji mbegu bora.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wakulima wa mpunga wakipewa mafunzo ya uzalishaji mbegu bora.

WADAU wa kilimo wametakiwa kujitokeza kutoa elimu ya uzalishaji mbegu kwa wakulima wa mpunga ili kuondokana na changamoto ya uzalishaji mbegu nchini, kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo Wilaya ya Bagamoyo Gerald Mwamuhamula wakati wa mafunzo ya siku tatu ya uzalishaji wa mbegu za ubora wakuazimia (UKU) za mpunga iliyofanyika wilayani Bagamoyo.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na  Taasisi ya  Kimataifa ya Utafiti wa Mpunga( IRRI) na kuvikutanisha vikundi vya uzalishaji mbegu kutoka mikoa mbalimbali.

Mwamuhamila alisema ni wakati wa wadau sasa kujitokeza na kuokoa sekta hiyo kwakufundisha wakulima kutengeneza mbegu ambazo zitazalisha mpunga bora.
 
"Lengo la mafunzo hayo  ni kwa ajili ya kuzalisha Mbegu za kuazimia ubora na kufanya hivyo ni kutatua changamoto  ya upungufu wa mbegu za mpunga ambayo ipo inawakabili wakulima mbalimbali, alisema.

Alisema wazalishaji wa mazao yakiwemo mpunga ni wengi nchini lakini suala la mbegu zenye ubora limekuwa changamoto na badala yake wengi wamekuwa wakizalisha mpunga kwa mbegu zinajirudia  na kusababisha uzalishaji  unakuwa chini tofauti na mwanzo.

Alisema baada ya mafunzo hayo wanatarajia wakulima hao watakaozalisha mbegu zinakuwa na idhini ya Wakala wa Mbegu nchini (ASA)  pia wanaoruhusu matumizi bora ya mbegu na Taasisi ya Kudhibiti Ubora  wa Mbegu Nchini (TOSCI).

Ofisa Miradi wa Shirika la Maendeleo  ya Kilimo Afrika Mashariki,  Robert Mwalubeke alisema lengo la mafunzo hayo ni kuandaa wazalishaji  mbegu hasa zenye ubora kwakuwa kuna changamoto ya upatikanaji wa mbegu na kuwafikia wakulima kwenye mabonde waliopo.