MRADI wa upanuzi wa uwanja wa Ndege Ibadakuli katika Manispaa ya Shinyanga, mkoani hapa unatarajiwa kukamilika Aprili mwakani na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Hayo yalibainishwa juzi na Mhandisi Ruburi Kahatano wa Kampuni ya Chico, inayotekeleza mradi wa ujenzi huo, wakati wa ziara ya waandishi wa habari mkoani hapa.
Kahatano, alisema ujenzi wa uwanja huo umefikia asilimia 80 na kwamba utakamilika kulingana na mkataba. Alisema hadi sasa kuna ndege mbili za dharura zimetua, moja kwa ajili ya kubeba mgonjwa kumpeleka Hospitali ya Mloganzila jijini Dar es Salaam.
Alisema mgonjwa huyo alitakiwa kwenda kupata matibabu zaidi ya kibingwa na kuokoa maisha yake.
Kahatano, alisema ndege nyingine ilitua uwanjani hapo kwa ajili ya kumleta mfanyakazi wa kampuni moja mkoani hapa.
“Uwanja huu kwa ndege mchana zinaweza kutua, lakini usiku haziwezi sababu bado hatujafunga taa,”alisema.
Mhandisi Chiyando Matoke wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga, wasimamizi wa ujenzi wa uwanja huo, alisema hadi kukamilika, utagharimu Sh.bilioni 44.8.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga, Greyson Kakuru, alisema katika ziara hiyo wameshuhudia kazi kubwa ambayo inafanywa na serikali ya ujenzi wa miradi ya kimkakati.
Kakuru, alisema kukamilika kwa upanuzi wa uwanja huo, kutafungua fursa za kiuchumi katika mkoa huo wa Shinyanga.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED