RITA yamaliza mgogoro wa msikiti

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 11:19 AM Dec 18 2024
Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi.
Picha: Mtandao
Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi.

WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), umeitaka Bodi mpya ya Wadhamini wa Msikiti wa Ijumaa, Mwanza, kujiepusha na ubadhirifu wa mali za msikiti sambamba na kuimarisha mshikamano miongoni mwa waumini.

Pia bodi hiyo imeagizwa kuacha kulipiza  visasi kwa bodi ya wadhamini ya msikiti huo iliyovunjwa. 

 Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi kwa bodi mpya ya msikiti huo, Kabidhi Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi, alisema uteuzi wa bodi hiyo mpya umetokea baada ya kuwapo kwa mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 30, baada ya kufanyika usajili wa mabadiliko ya katiba mwaka 1990.

 “Sababu zinazotajwa kusababisha migogoro hiyo ni kutotambulika mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1993 yaliyowasilishwa kwa Msajili Mkuu mwaka 1997, kutoelewana wajumbe wa bodi ya wadhamini iliyokuwapo, matumizi mabaya ya mali, fedha na kukosekana kwa uwazi katika taasisi,” alisema Kanyusi.

Alisema Februari 2, mwaka huu, RITA iliunda kamati ya uchunguzi ambayo ilifanya kazi kwa kipindi cha mwezi mmoja na kukabidhi ripoti iliyoonesha kuna ubadhirifu wa takribani Sh. bilioni moja.

“Baada ya tuhuma zilizokuwa zikiikabili bodi iliyopita, niliunda kamati ya uchunguzi iliyowasilisha taarifa kwa mamlaka za uchunguzi (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa - TAKUKURU). Mpaka sasa kazi imeshaanza kufanyika na baadhi ya wajumbe wa bodi iliyopita wameshahojiwa. 

Hivi punde TAKUKURU itakamilisha kazi yake na watakaobainika katika ubadhirifu huo taratibu za kisheria zitafuatwa ili kila mmoja apate stahiki kwa mujibu wa sheria.” Alisema Kanyusi.

Kanyusi alitoa rai kwa wajumbe wa bodi mpya ya udhamini kutekeleza majukumu yao kama sheria inavyotaka na kusisitiza kuwa wao si wamiliki wa mali bali ni wasimamizi kwa niaba ya wanachama, hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa ujibu wa sheria.

Makamu Mwenyekiti Bodi Mpya ya Wadhamini ya Msikiti wa Ijumaa, Sherally Hussein, mbali na kuipongeza RITA kwa usimamizi mzuri, alisema wakati umefika wa kuunganisha nguvu kwa Waislamu wote wa msikiti huo ili usimamia malengo yaliyokusudiwa kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

“Kwa sasa tuna imani kwani ile mivutano iliyotugawa kwa makundi tofauti tofauti imekwisha. Ni wakati sahihi sasa makundi yote kuungana ili taasisi yetu itoe mchango stahiki kwa waumini wote na taifa kwa ujumla wake,” alisema Hussein.

Kanyusi aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa bodi mpya ya wadhamini katika uongozi ili iweze kutimiza majukumu yake kikamilifu kwa maslahi mapana ya waumini wa jumuiya ya Kiislam mkoa wa Mwanza.