Mil. 800/- kuwainua kiuchumi vijana wa mikoa mitatu nchini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:34 AM May 24 2024
Mkataba huo umesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini, Shigeki Komatsubara makao makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkataba huo umesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini, Shigeki Komatsubara makao makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam

DOLA za Marekani 300,000 (Sh. milioni 800) zitatumika kuwainua kiuchumi vijana kutoka mikoa mitatu nchini katika ushirikiano mpya kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) na Taasisi ya CRDB Bank Foundation.

Katika kuongeza ujumuishi wa wananchi kiuchumi hasa makundi maalum, taasisi hiyo imetia saini mkataba wa makubaliano kushirikiana na UNFPA kuwawezesha kiuchumi vijana wa umri wa kuanzia miaka 18 hadi 24 walioko shuleni na wale ambao wameacha shule kutokana na sababu mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya kutia saini mkataba huo wenye thamani ya Dola 300,000 za Marekani (Sh. milioni 800) jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa alisema ushirikiano huo unatokana na kufanana kwa malengo na mipango ya pande zote mbili katika kuwezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi.

"Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023, Taasisi yetu ya CRDB Bank Foundation tumeelekeza nguvu kubwa katika kuanzisha programu za kuwawezesha vijana na wanawake kujumuishwa kwenye mfumo rasmi wa huduma za fedha, kuwapa mafunzo na mitaji wezeshi kupitia Programu yetu ya Imbeju. Ushirikiano huu na UNFPA unakwenda kuimarisha jitihada hizi na kuwezesha kufikia vijana wengi zaidi," alisema Tully.

Kama ilivyo kwa taasisi hiyo, UNFPA inatekeleza programu tofauti za kuinua wananchi kiuchumi, kuwajengea uwezo wa kuzitambua haki zao, kupunguza migogoro ya kifamilia na kijinsia pamoja na kutoa elimu ya uzazi kwa wanawake, mabinti na vijana, azma ikiwa ni kujenga vijana wenye uwezo wa kiuchumi kukabili changamoto za kila siku.

Tully alisema ushirikiano huo unalenga vijana walio masomoni na wale walioshindwa kuendelea na masomo kutokana na sababu mbalimbali, watu wenye ulemavu pamoja na mabinti waliopata ujauzito wakiwa masomoni. 

Katika utekelezaji wake, alisema wanakusudia kupunguza changamoto za upatikanaji ajira, kuwapa elimu ya fedha, kuwapa elimu ya afya ili kupunguza mimba za utotoni, kupunguza ukatili wa kijinsia na maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) katika mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Dodoma na Kigoma.

"Ushirikiano wetu na UNFPA utajikita kwenye maeneo mawili ya msingi. Kwanza ni kutoa elimu na maarifa ya kujitambua kwa vijana walio shuleni na walioa nje ya shule itakayojumuisha mafunzo juu ya huduma rafiki za afya, unyanyasaji kijinsia na jinsi ya kuepuka na namna ya kuishi na maambukizi ya VVU. 

"Eneo la pili ni kutoa elimu ya fedha na ujasiriamali kwa vijana na mabinti ili kuwajengea mazingira ya kutekeleza majukumu yao kikamilifu," Tully alieleza.

Mark Bryan Schreiner, Mwakilishi Mkazi wa UNFPA nchini, alisema shirika hilo limekuwa linatekeleza miradi tofauti inayolenga kuwainua wananchi hasa wa makundi yaliyosahaulika katika jamii ili kuwa na uchumi jumuishi na wanufaika wakubwa wa programu zake ni wanawake, vijana wakiwamo mabinti wenye rika la balehe na wahamiaji wanaoomba hifadhi kutokana na migogoro ya kisiasa na kijamii inayotokea kwenye mataifa jirani.

"Tukiangalia changamoto zinazowakabili vijana nchini ikiwamo upatikanaji mitaji, ukosefu wa ajira na elimu  ya ujasiriamali, UNFPA inayo kila sababu ya kushirikiana na wabia wa kimkakati kusaidia kuwezesha vijana nchini kushiriki kujenga uchumi wa taifa lao," alisema Schreiner.

Alisema UNFPA inatekeleza programu yake ya tisa nchini inayohamasisha uzazi salama kwa kuitambua na kuikubali kila mimba inayopatikana pamoja na kumwezesha kila kijana kutimiza ndoto za maisha yake.  

"Lengo letu ni kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma, hivyo tunashirikiana na wadau wenye mtazamo kama wetu kama ilivyo Taasisi ya CRDB Bank Foundation," alisema Schreiner.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, zaidi ya nusu ya Watanzania ni vijana wenye umri chini ya miaka 24. 

Matokeo ya sensa hiyo pia yanaonesha asilimia 44 ya watu wote ni watoto wenye umri chini ya miaka 15 huku asilimia 19 wakiwa vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 24. Ndiyo idadi kubwa ya wananchi watakaoguswa na mradi huo wa kwanza wa ushirikiano kati ya CRDB Bank Foundation na UNFPA.