MKUU wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela amesema mifumo ya uuzaji mazao ya nafaka na mazao mchanganyiko itaimarisha ukuaji wa sekta ya kilimo na kumlinda mkulima dhidi ya unyonyaji kwenye bei na vipimo.
Shigela alisema hayo mjini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kukutana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Irene Mlola wakati wa ziara yake ya kikazi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Alisema Geita inaunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kupitia COPRA katika kurasimisha biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko kwa kuweka mazingira ya kuhakikisha mkulima ananufaika na kazi ya mikono yake.
"Geita tunaunga mkono jitihada za Serikali kupitia COPRA, hivyo tutaendelea kushirikiana ili kuhakikisha wakulima wananufaika na uwepo wa mamlaka hiyo,"alisisitiza Shigela.
Alisema wao kama serikali ya mkoa watatoa ushirikiano kwa maofisa wa COPRA katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku mkoani Geita.
Aliwataka wakulima na wafanyabiashara wa mazao wa Geita kutoa ushirikiano kwa maofisa COPRA watakapohitajika.
Kwa upande wake, Irene, alisema mamlaka hiyo imeanza kuweka wataalamu wake watakaoshirikiana na wengine mikoa ya kanda hiyo kuhakikisha biashara ya nafaka na mazao hayo inafanyika kwa kufuata mifumo ilivyoelekezwa na serikali.
Alisema wataalam hao watafanya kazi kwa kuhakikisha mazao yote yanayozalishwa katika mikoa hiyo yanakuwa na ubora wa hali ya juu unaohitajika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Irene, alimshukuru Shigela kwa ushirikiano aliowapa na kusisitiza COPRA italeta mageuzi makubwa kwa wakulima na kunufaika kiuchumi.
Alisema atahakikisha wataalam wa COPRA wanafanya kazi kwa weledi kwa kushirikiana na wataalam wa sekta ya kilimo kuanzia ngazi ya vijiji hadi mkoa na kuleta matokeo chanya kwa wakulima na taifa.
Mkurugenzi huyo wa COPRA anaendelea na ziara ya kikazi katika mikoa hiyo baada ya kukamilisha baadhi ikiwamo Simiyu, Kagera na Geita.
Ziara hiyo ina lengo la kutambulisha mamlaka hiyo, mkurugenzi huyo, maofisa wake na kuweka mazingira ya utendaji kazi wa pamoja ili kuendesha shughuli za biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko yanayolimwa huko.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED