Mhagama azindua huduma saba BMH

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 07:09 AM Sep 15 2024
Mhagama azindua  huduma saba BMH
Picha: Mtandao
Mhagama azindua huduma saba BMH

WAZIRI wa Afya, Jenista Mhagama, amezindua huduma saba katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) vikiwamo vyumba vya upasuaji vinavyotembea ambavyo vitaendelea kuimarisha huduma za afya kwa jamii nchini.

Huduma nyingine ni pamoja na kutengeneza miguu bandia, miongozo ya matibabu, kitengo cha huduma kwa wateja, maabara maalum, vyumba vipya vya  upasuaji, miongozo  ya idara ya kutoa huduma.

Akizungumza juzi katika uzinduzi huo, Mhagama aliagiza zitumike ipasavyo kwa jamii, huku akiwapongeza watumishi hospitalini huko kwa ubora wa huduma za afya wanazotoa.

 "Ninampongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali, Prof. Abel Makubi, na timu nzima ya watumishi wenzake kwa huduma nzuri na ufanisi katika kuboresha huduma za afya,” alisema.

Waziri Mhagama alisema BMH ni hospitali kubwa, hivyo inapaswa kuendelea kujitangaza kwa kutoa huduma bora ndani na nje ya nchi.

Kila huduma aliyoizindua, alisema  ina kazi maalum, na kuagiza watumishi kuzitumia vizuri ili uwekezaji wa serikali kwenye sekta ya afya ufanyike.

Alisema serikali inahitaji kuona huduma za afya zinatolewa kwa jamii ipasavyo kutokana na uwekezaji unaofanywa.

Prof. Makubi alisema watumishi hospitalini hapo wameshirikishwa katika kuandaa Standard Operating Procedures (SPO) ‘Taratibu za Kawaida za Uendeshaji’

 “Ninawasifu sana watumishi wangu wa BMH wameshiriki kikamilifu katika kuandaa SPO ambazo zitatuongoza katika kutoa huduma,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya BMH, Dk. Deodatus Mtasiwa, alisema uanzishwaji wa hospitali hiyo umetokana na muhtasari wa hospitali kama saba za India.

“Hata mchoraji wa Hospitali hii ni mtanzania baada ya kuangalia muhtasari wa hospitali saba za India," alisema Dk. Mtasiwa.