DC aagiza shule zote za serikali zipande miti isiyopungua 100

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 05:14 PM Sep 21 2024
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda wapili kushoto, Ofisa Misitu Temeke Neema Daudi wakwanza kushoto, Mkurugenzi Mtendaji wa Bima ya Afya ya Jubilee Dk. Harold Adamson wapili kulia, wakipanda miti katika Shule ya Msingi Madenge.
Picha Maulid Mmbaga.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda wapili kushoto, Ofisa Misitu Temeke Neema Daudi wakwanza kushoto, Mkurugenzi Mtendaji wa Bima ya Afya ya Jubilee Dk. Harold Adamson wapili kulia, wakipanda miti katika Shule ya Msingi Madenge.

MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Sixtus Mapunda, ameziagiza shule zote za serikali kuhakikisha kwamba zinapanda miti angalau isiyopungua 100 ikijumuisha ya matunda na kivuli, ili kuongeza chachu ya utunzaji mazingira.

Pia ametoa wito kwa wanajamii kuachana na desturi ya kuweka sakafu katika maeneo makubwa yanayozunguka makazi yao badala yake wapande maua na miti itakayosaidia kufyonza maji nyakati za mvua na kuepusha mafuriko, akieleza kuwa sakafu zinasababisha maji yakose pa kwenda.

Mapunda, ameyabainisha hayo mapema leo wakati wa zoezi la upandaji miti lililoratibiwa na bima ya Afya na Maisha ya Jubilee na taasisi ya Agakhan katika Shule ya Msingi Madenge iliyoko wilayani humo, ambako mkuu huyo ameongoza upandaji miti 200.

"Wanafunzi wote wanapaswa kuona umuhimu wa utunzaji mazingira kwa kila mmoja kupewa mti wake aulee toka darasa la kwanza hadi saba, tusisingizie maendeo, kuna watu majumbani kwao wanaweka sakafu uwanja mzima wewe haupumui ardhi haipumui.

"Tukianza kwa mwanafunzi akiwa na tabia ya kupanda miti kuanzia shule ataipeleka hadi nyumbani, mimi naamini tukiamua kweli ndani ya miaka mitatu Dar es Salaam itakuwa tofauti kwa kiwango cha juu, ukiwa Mbagara ukitoka kwenda Chamanzi unaweza kuona uko nchi nyingine," amesema Mapunda.

Ameongeza kwa kusisitiza watu kuacha tabia ya kupanda miti isiyokuwa na faida badala yake wapande ya matunda pamoja na mbogamboga ili wanafunzi wafaidike kwa chakula.

"Tubadilike tupande vitu vinavyotusaidia na tuache 'ushamba' wa kuweka sakafu kila mahali, hayo mambo yalishapitwa na wakati, zamani yalikuwa na tija lakini kwa sasa hayana faida kutokana na hali ya mabadiliko ya tabianchi," amesema Mapunda.

Pia ameshauri kuwekwa miundombinu mizuri itakayosaidia maji kupata pa kwenda nyakati za mvua ili kuepukama na athari za mafuriko katika jamii.

Hata hivyo, ameeleza kuwa serikali ina wajibu wa kutengeneza miundombinu lakini kila mwananchi anawajibu wa kulinda mazingira yanayomzunguka, akieleza kuwa endapo mtu hatazingatia mazingira yake na kusababisha maji kupiga hodi kwake asije akawalalamikia.

Vile vile, amewapongeza bima ya afya na maisha ya Jubilee na Agakhan kwa jitihada wanazozifanya kuisaidia serikali katika kutekeleza masuala mbalimbali yenye manufaa kwa jamii.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Bima ya Afya ya Jubilee, Dk. Harold Adamson, amesema upandajivwa miti hiyo ni muendelezo wa programu yao ya utunzaji wa mazingira kwa kuchagiza umuhimu wa kuongeza misitu.